Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo kisicho na suluba ndio jibu la kutokomeza njaa Afrika

Mbinu kama hizi za kusafirisha mazao kupeleka sokoni hazina tija kwa mkulima.
©FAO/Pius Utomi Ekpei
Mbinu kama hizi za kusafirisha mazao kupeleka sokoni hazina tija kwa mkulima.

Kilimo kisicho na suluba ndio jibu la kutokomeza njaa Afrika

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na Muungano wa Afrika, AU leo wamezindua mwongozo mpya utakaosaidia bara la Afrika kutumia zana za kisasa za kilimo na hivyo kuondokana na kilimo cha suluba kisicho na tija.

Uzinduzi wa mwongozo huo uliopatiwa jina SAMA umefanyika leo huko Roma, Italia na unafuatia majadiliano kati ya watunga será wa AU, FAO na wadau wa msingi.

Mathalani mwongozo huo unaweka bayana historia ya zana za kilimo barani Afrika na hatua za kuchukua ili kuweka fursa  mpya na kuhakikisha kuna hatua bora zaidi za kutumia zana mpya za kilimo Afrika.

"Kuongeza maradufu tija kwenye kilimo Afrika na kutokomeza njaa na utapiamlo barani  humo ifikapo mwaka 2025 itasalia ndoto iwapo matumizi ya mashine za kisasa kwenye kilimo hayatapatiwa kipaumbele cha juu kabisa,” amesema Josefa Sacko, kamishna wa AU kwa masuala ya uchumi wa vijijini na kilimo.

Amesema cha kusitikisha ni kwamba zaidi ya asilimia 75 ya wakulima barani Afrika wanatumia zana duni kama vile jembe la mkono au lile la kukokotwa kaw ng’ombe ili kuandaa mashamba yao, hali ambayo inasababisha uzalishaji mdogo licha ya suluba nyingi wanazopitia kwenye kilimo hicho.

Mkulima  akiandaa shamba kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe huko Bahir Dar Ethiopia.
Photo: FAO/Giulio Napolitano
Mkulima akiandaa shamba kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe huko Bahir Dar Ethiopia.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Maria Helena Semedo amesema wakulima barani Afrika wanapaswa kuwa na uwezo wa kutumia zana za kisasa za kilimo, ziwe mashine zinazoonekana au teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalisaji kwenye sekta hiyo kwa njia endelevu.

"Kuongeza maradufu tija kwenye kilimo Afrika na kutokomeza njaa na utapiamlo barani  humo ifikapo mwaka 2025 itasalia ndoto iwapo matumizi ya mashine za kisasa kwenye kilimo hayatapatiwa kipaumbele cha juu kabisa

Mwongozo huo mpya unaainisha vipaumbele 10 vya AU ikiwemo mipango ya kitaifa, kuanzia mahitaji ya kuwa na mashine za kisasa, vipuri na mifumo bunifu ya kuchangisha fedha na umuhimu wa ushirikiano wa kikanda unaoweza kuhamisha utaalamu kutoka nchi moja hadi nyingine.

Halikadhalika unasisitiza kuwa mikakati hiyo lazima ihusishe mfumo mzima wa kilimo kuanzia kulima, kuvuna, kushughulikia mavuno, mchakato wa mazao na uhifadhi ili kupunguza upotevu wa chakula.

Kwa mantiki hiyo mfumo unataka kuunganishwa kati ya mkulima na mlaji.