Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Imarisheni huduma vijijini ili vijana washiriki kwenye kilimo- FAO

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano wa kikanda kuhusu vijana na kilimo mjini Kigali Rwanda.
FAO/Luis Tato
Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano wa kikanda kuhusu vijana na kilimo mjini Kigali Rwanda.

Imarisheni huduma vijijini ili vijana washiriki kwenye kilimo- FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Hatua za dhati zinahitajika ili vijana wa Afrika waone kilimo kuwa ndio muarobaini wa changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO Jose Graziano da Silva.

Bwana Da Silva amewaeleza washiriki wa mkutano wa kimataifa  kuhusu ajira kwa vijana kwenye sekta ya kilimo unaofanyika mjini Kigali, Rwanda, kuwa bila hivyo vijana wataendelea kuona kilimo kama mateso na si suluhisho.

“Mahitaji ya chakula barani Afrika yanatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 miaka michache ijayo kutokana na ongezeko la idadi ya watu,  ukuaji wa miji na mabadiliko ya mlo kwenye kaya kutokana na ongezeko la vipato,” amesema Bwana Da Silva akisema kuwa sekta ya kilimo cha biashara inatarajiwa kuwa na thamani ya dola trilioni Mojam waka 2030.

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima kuweka mazingira bora kama kuimarisha teknolojia na mbinu za kilimo huko vijijini ambako  hivi sasa vijana wanakimbia kutokana na  ukosefu wa huduma hizo.

“Katika miaka ijayo, shughuli nyingi zaidi za kilimo pamoja na ajira kwenye sekta hiyo vitahitaji stadi za kidijitali. Vyama vya ushirika na makundi mengine ya ushirika yanawasilisha njia bora zaidi za kupatiwa familia na vijana msaada wa stadi za ufundi, kuwajengea uwezo na kupata teknolojia za kisasa zitumikazo kwenye kilimo,” amesema mkuu huyo wa FAO.

Sekta ya kilimo nayo  yaajiri watu wengi. Vijana wanaombwa wahusishwe katika kilimo.
FAO/Olivier Asselin
Sekta ya kilimo nayo yaajiri watu wengi. Vijana wanaombwa wahusishwe katika kilimo.

 

Amesisitiza kuwa ni lazima kufikiria zaidi ya kazi za mashambani na kuibuka na mbinu na fursa katika mlolongo mzima kuanzia kwenye uzalishaji wa mazao hadi usambazaji wa mazao hayo kwa watumaiji. “Ongezeko la bidha bora zaidi za mashambani huko mijini linaongeze fursa nyingi za ajira katika uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa mazao ya kilimo pamoja na masoko na biashara ya rejareja,” amefafanua Bwana Da Silva.

Hata hivyo amesema jambo muhimu ili vijana wakubali kufanya kazi hizo ni kuweka mabadiliko huko vijijini kwa kuhakikisha kuna huduma bora za msingi kama vile afya, elimu, umeme, intanent na kadhalika akisema kuwa kwa kufanya hivyo vijana watachangia katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kupitia sekta ya kilimo.

Mkutano huo wa kimataifa utamalizika kesho.