Kenya yachukua hatua mahsusi ili vijana washike hatamu za taifa

5 Agosti 2019

Nchini Kenya serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kuwa suala la uwezeshaji vijana katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs linatekelezwa kivitendo badala ya kusalia kwenye makaratasi.

Hatua hizo zinazochukuliwa zimewekwa bayana na Maureen Mutai, mjumbe wa bodi ya ushauri ya vijana kwenye ofisi ya Rais wa Kenya wakati alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, pindi aliposhiriki mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kuhusu ajenda ya vijana, amani na maendeleo.

Bi. Mutai amesema kwanza wanasaka majukwaa, “mahali vijana watazungumza shida zao wanaweza kuzungumza kwa idara tofauti za serikali ambazo zinawakandamiza ili tuweze kufahamu wapi tunakwenda vibaya na ili tuweze kutimiza mahitaji yao na kuwasikiliza na kuwaboresha kimaisha kwa sababu wao ndio viongozi wa sasa. Na kama tunataka taifa lisonge mbele tunafaa kuwaanzishia hatua sasa hivi ili kusiwe na pengo. Na hilo ndio jambo tunataka sasa vijana wapate uzoefu ili waweze kushikilia taifa hivi karibuni na kuendeleza uchumi sasa na taifa lenyewe.”

Alipoulizwa ni jambo gani linamtia moyo zaidi, Bi. Mutai amesema “nafurahi mahali ambapo tumefika kama taifa na zaidi kama Afrika. Kuna wakati hatukuwa na vijana ambao wanaweza kusimama au kuja na ujumbe wa serikali kwenye mkutano mkubwa. Na sasa hivi tunaona hata kama hatuhafika mahali tunataka, angalau tumeanza na tumeanza mahali, na sasa tuko na nafasi na mahali ya kuboresha wale wengine ambao hawana hii nafasi lakini wana  sauti.”

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter