Kisa cha nne cha ebola charipotiwa Goma, DRC

2 Agosti 2019

Kisa cha nne cha ugonjwa wa ebola kimeripotiwa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Uswisi kwa njia ya simu kutoka DRC msemaji wa WHO, Margaret Harris amesema wanaendelea kufuatilia historia ya usafiri wa mgonjwa katika siku chache zilizopita ili kubaini alikoambukizwa mgonjwa huyo. Kwa mujibu wa tarifa kutoka WHO Julai 31 mwaka huu kumekuwa na visa 2713 huku 2619 vikiwa vimethibitishwa na vingine 94 vinashukiwa, ikiwemo vifo 1823, na manusura 771 ambao wanaendelea kupokea matibabu.

Kama sehemu ya kufuatilia hali inayomhusisha mtoto huyu aliyeambukizwa ebola, bi.Harris ameongeza kwamba WHO imegundua takriban watu 200 ambao walikutana na muathirika na sasa ni suala la kuhakikisha kwamba tunagundua kwa haraka kesi mpya za maambukizi.

Afisa huyo wa WHO amesema lengo ni kuhakikisha kwamba watu wote ambao walikuwa karibu na mgonjwa wanajulikana na kuchanjwa katika muda wa saa 24 au ndani ya saa 48.

WHO pia inalenga kuwachanja watu ambao wako karibu na watu walikutana na mtoto huyo, pia kuhakikisha usalma wa maeneo waliko wagonjwa na ufuatiliaki wa wapi mgonjwa alipita.

WHO inapendekeza mipaka ya DRC na nchi jirani isalie wazi

Bi. Harris ameongeza kwamba, “WHO imekuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa ugonjwa kuja Goma, kwani ni mji wa takriban watu milioni 2.” Goma sio tu ni mpaka na Rwanda lakini ni kituo cha usafiri nchini na nje ya nchi.

Licha ya hali ya sasa Goma, WHO imesema suala la kufunga mipaka halina matokeo chanya, “WHO kwa kuzingatia mapendekezo ya kamati yake kuhusu maswala ya dharura haijapendekeza kufungwa kwa mipaka au kuweka vizuizi dhidi ya usafiri au biashara kwani hili linaweza kuzua taharuki na kusababisha watu walio na dalili za ugonjwa kujificha na kuendelea na shughuli zao za kila siku, “ amesema Bi. Harris, akiongeza kwamba, hilo linafanya ugunduzi wa virusi kuwa mgumu.”

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Ebola, DRC

Wakati huohuo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limefanya kikao kujadili amani na Usalama barani Afrika likijikita zaidi na ebola inayoendelea kutoa changamoto DRC.

Baraza la Usalama kupitia tarifa iliyotolewa na rais wake kwa mwezi huu imerejelea wasiwasi wake kuhusu mlipuko wa hivi karibuni nchini DRC na kuzingatia kwamba WHO imetangaza mlipuko huo kuwa ni dharura ya umma ya kiafya nchini DRC na wasiwasi wa kimataifa.

Baraza la Usalama limesisitiza umuhimu wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa sababu uanweza kuenea kwa kasi ikiwemo nchi jirani na kuzua changamoto ya kibinadamu na kuathiri usalama wa ukanda huo.

Wajumbe wa baraza hilo wamerejelea kutoa shukrani zao kwa juhudi za serikali ya DRC, WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Matiafa pamoja na ujumbe wa Umoja huo nchini DRC, MONUSCO na muungano wa Afrika, mashirika ya misaadaya kibinadamu na wafadhili wa kimataifa kwa mchango wao katika kukabiliana na ugonjwa na kutibu wagonjwa.

Aidha baraza la usalama limesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikian na DRC kukabiliana na mlipuko wa ebola pamoja na mataifa kwenye ukandao huo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter