Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani shambulio la karibuni zaidi nchini Nigeria

Watoto kutoka katika familia zilizoparaganyika katika eneo la Maiduguri, jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria wakikinga maji. Mgogoro katika eneo hilo umewalazimisha mamia ya maelfu kuyahama makazi yao na kuishi kwa kutegemea misaada.
UNICEF/Gilbertson VII Photo
Watoto kutoka katika familia zilizoparaganyika katika eneo la Maiduguri, jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria wakikinga maji. Mgogoro katika eneo hilo umewalazimisha mamia ya maelfu kuyahama makazi yao na kuishi kwa kutegemea misaada.

UN yalaani shambulio la karibuni zaidi nchini Nigeria

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la hivi karibuni zaidi lililofanywa jimboni Borno nchini Nigeria na kusababisha vifo vya raia.

Vyombo vya  habari vinaripoti kuwa shambulio hilo la mwishoni mwa wiki wakati wa mazishi kwenye jimbo hilo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria lilisababisha vifo vya watu wapatao 65, idadi ambayo yadaiwa ni mara tatu zaidi ya ile iliyokuwa imeripotiwa awali.

Habari zinasema kuwa maiti zaidi walipatikana siku ya Jumapili kufuatia shambulio hilo lililofanywa na watu wenye silaha kwenye mji wa Maiduguri, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Borno.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York, Marekani ametua salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Nigeria huku akitakia ahueni ya haraka manusura.

Halikadhalika ametaka wahusika wa shambulio hilo wafikishwe haraka mbele ya sheria.

Katibu Mkuu ametoa wito wa kukomeshwa haraka kwa visa vya aina hiyo akisema vinatishia usalama wa binadamu na kinyume na haki za kibinadamu.

Halikadhalika Katibu Mkuu ameelezea mshikamano wa Umoja wa Mataifa na serikali na watu wa Nigeria katika juhudi zao za kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali.

Eneo hilo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria mara kwa mara limekuwa likikumbwa na mashambulizi kutoka kikundi cha kigaidi cha Boko Haram na hadi sasa hakuna kikundi chochote kilichodai kuhusika na shambulio hilo la karibuni zaidi.