Shime sasa tuongeze kasi tunusuru wanawake Afghanistan- Bi. Mohammed

26 Julai 2019

Wanawake nchini Afghanistan wameendelea kubeba mzigo zaidi wa madhara yatokanayo na mzozo uliodumu nchini humo takribani miongo minne sasa, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed wakati akihutubia Baraza la Usalama la umoja huo hii leo jijini New York, Marekani.

Hotuba yake hiyo inafuatia ziara yake ya siku mbili nchini humo mwishoni mwa wiki iliyopita ziara ambayo ilimkutananisha na makundi mbalimbali kwenye mji mkuu Kabul na pia jimboni Barmyan.

Bi. Mohammed alianza hotuba yake hiyo kwa kutuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Afghanistan kufuatia shambulio la jana nchini humo, akisema “mashambulizi ya kiholela yamekuwa yanaya wanawake na watoto na yamekuwa kinyume cha ubinadamu na ni uhalifu chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa katika tukio hilo la jana, watu wapatao 15 waliuawa kufuatia mashambulizi matatu kwenye mji mkuu Kabul ambao bomu moja lililenga basi lililokuwa limebeba wafanyakazi wa serikali.

Amesema Umoja wa Mataifa unasimama kidete na wananchi wa Afghanistan wakati huu ambapo wanajitahidi kusaka amani ya kudumu nchini mwao.

Akirejelea ziara yake hiyo ambayo aliambatana na viongozi wengine waandamizi wa Umoja wa Mataifa akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women Phumzile Mlambo-Ngcuka na lile la idadi ya watu, UNFPA,  Natalia Kanem, Naibu Katibu Mkuu amesema katika maeneo ambayo wataliban wameshika tena hatamu za uongozi, “kuna ripoti za mauaji ya kutolewa kafara, wanawake kuuawa kwa kupigwa mawe na hata haki zao kukiukwa.”

Bi. Mohammed amesisitiza kuwa amani, usalama na utulivu wa kiuchumi vinahitajika haraka ili kuweza kunusuru kundi hilo.

Naye Mkuu wa idara ya siasa ya Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo ambaye pia alikuwepo ziarani Afghanistan amewaambia wajumbe kuwa, “suluhu la kisiasa nchini Afghanistani linasalia kuwa muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule, wakati huu ambapo raia wanaendelea kubeba mzigo wa mzozo unaoendelea.”

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter