Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wengi wauawa kwenye shambulio Afghanistan

Kaimu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Toby Lanzer asema hana shaka kuwa shambulio la leo limelenga raia makusudi. (Picha:UNAMA)

Watoto wengi wauawa kwenye shambulio Afghanistan

Nchini Afghanistan, shambulio kwenye kitongoji cha Qalai Nazir karibu na mji mkuu Kabul, limesababisha watu wapatao 100 kuuawa na wengine wengi wamejeruhiwa.

Kaimu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMA, Toby Lanzer amesema hana shaka kuwa shambuli hilo lililenga raia waliokuwa wamejumuika kwenye kituo cha utamaduni cha waislamu wa madhehebu ya Shia.

Yaelezwa kuwa idadi kubwa ya waliopoteza maisha ni watoto na kwamba hali ilivyo yasemekana idadi hiyo itaongezeka.

Bwana Lanzer amesema shambulio hilo linaweza kuwa uhalifu dhidi ya kibinadamu ambapo tayari wanamgambo wa kikundi cha ISIL au Daesh wamekiri kuhusika nalo.

Kaimu mkuu huyo wa UNAMA ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa huku akisema kuwa shambulio la leo linaimarisha zaidi azma yao ya kushirikiana na wananchi wa Afghanistani ambao wanataka amani irejee nchini mwaka mwaka 2018.