Somalia bado inahitaji msaada wa kimataifa kupambana na changamoto za haki-Nyanduga

25 Julai 2019

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Somalia Bahame Tom Nyanduga akiwasilisha taarifa yake hii leo mjini Geneva Uswisi baada ya ziara yake mjini Mogadishu Somalia amesema, jumuiya ya kimayaifa inapaswa kuendelea kuisaidia Somalia kuimarisha taasisi zake na sekta ya sheria na usalama wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi.

“Somalia imepiga hatua kubwa katika hali ya siasa, uchumi, jamii na haki za binadamu katika kipindi cha miaka sita iliyopita lakini bado kuna mengi ya kufanya.” Ameeleza Bwana Nyanduga.

Aidha ameisihi jumuiya ya kimataifa na serikali kuu ya Somalia kushughulikia matokeo mabaya ya mabadiliko ya tabianchi yanayowaathiri watu, na kuhakikisha kunakuwa na haki za msingi za binadamu kama vile maji, huduma za afya na elimu kwa watoto wote hususani wasichana.

“Somalia pia inakabiriana na changamoto nyingine zikiwemo mgogoro unaoendelea, kukosekana kwa usawa, ubaguzi na ukosefu wa ajira kwa vijana, pia usambazaji wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.” Bwana Nyanduga amesisitiza.

Mtaalamu huyo huru amewapongeza watu wa Somalia kutokana na uimara wao katika kipindi cha mgogoro, mashambulizi ya mabomu ya kigaidi, majanga ya asili, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na changamoto nyingine kama vile umaskini na ukosekanaji wa mahitaji muhimu kwa ustawi wao.

Nyanduga pia amekaribisha hatua ya Somalia kutekeleza mkataba wa haki za watu walio na ulemavu.

Wakati wa ziara yake ya siku 12, Nyanduga alienda Mogadishu, Hargeisa na Nairobi na amefanya mazungumzo na selikali kuu ya Somalia na Somaliland, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, AMISOM, jamii ya wafadhili na jumuiya za kiraia.

Taarifa kamili ya ziara ya mtaalamu huyo itawasilishwa katika ripoti ya kina ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2019.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter