Angalau sasa wigo wa upigaji kura Somalia umekuwa mpana tofauti na awali- Nyanduga

25 Oktoba 2019

Mtaalamu huru wa haki za binadamu kwa Somalia, Bahame Tom Nyanduga, ametoa tathmini yake ya hali ya haki za binadamu nchini humo hususan suala la uchaguzi, wanawake na watoto  kwenye taifa hilo la Afrika, akisema hali angalau sasa kuna matumaini zaidi ikilinganishwa na hapo awali. Priscilla Lecomte na ripoti kamili.

Bahame Tom Nyanduga, mtanzania ambaye mwishoni mwaka huu anatamatisha jukumu lake la kuwa mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu nchini Somalia.

Wiki hii amewasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ripoti yake ya mwaka kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Somalia, ikiangazia masuala kadhaa ambapo nilimuuliza vipi hali ya haki za binadamu hususan ushiriki wa uchaguzi?

Katika hilo, Bwana Nyanduga amesema, “utaona kwamba pale mwanzoni serikali ilikuwa bado inaaanza kujizatiti kwa sababu walikuwa wamechaguliwa mwaka 2012. Lakini baada ya hapo kumefanyika chaguzi, uchaguzi ambao ulihusisha wajumbe wengi zaidi. Kwa sababu awali waliochagua serikali walikuwa ni kundi la wazee wasiozidi zaidi ya 130 na kitu. Lakini baada ya mfumo mpya waliojiamuliwa, waliweza kupata wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za Somalia ambao walikuwa karibu ya 12, ambao waliweza kuchagua wabunge mwaka 2016 na mwaka 2017 wakamchagua Rais.”

Kwa mantiki hiyo amesema kwa hivi sasa serikali iliyoni kwanza ni kielelezo ya kwamba kwa upande wa kimfumo wa kiutawala wameweza kuongeza jitihada kwa sababu “kama nilivyosema hapo awali kulikuwa na udhaifu lakini sasa unaona serikali imezidi kujizatiti.”

Mbunge katika bunge la Somalia, akipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2017. Katika mabadiliko ya katiba uchaguzi ujao utakuwa mtu mmoja kura moja.
UN Photo/Ilyas Ahmed
Mbunge katika bunge la Somalia, akipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2017. Katika mabadiliko ya katiba uchaguzi ujao utakuwa mtu mmoja kura moja.

Kisha nikataka kufahamu pamoja na kuongezeka kwa idadi  ya wapiga kura, vipi ushiriki wa wanawake katika kupiga kura na kushika nafasi za uongozi ambapo Bwana Nyanduga amesema kwamba, “Somalia imepiga hatua kubwa ukizingatia hasa wakati wa zoezi la uchaguzi la mwaka 2016, wanawake walijitokeza kama washiriki katika kupiga kura, iadi ya washiriki iliongezeka kutoka zaidi ya 100 hadi takribani 12,000, wanawake walikuwa washiriki katika kupiga kura. Na katika hilo idadi ya wanawake bungeni iliongezeka na kufikia karibu asilimia 25. Kwa hiyo, hali hiyo ukizingatia kuwa ni uchaguzi uliofanyika katika mazingira yasiyo salama, ilikuwa ni hatua kubwa sana.”

Ameendelea kusema kuwa,  “serikali kwa kutambua hilo, rais aliwateua wanawake watano na kuwapa nyadhifa muhimu sana, zikiwemo nyadhifa ya kusimamia bandari ya Mogadishu, na kama unavyofahamu bandari ya Mogadishu ni kitengo muhimu sana katika uchumi wa Mogadishu. Mwingine ni mama ambaye amekuwa anaongoza katika masuala ya haki za binadamu  ambaye ndiye Waziri na mshirika wangu katika kuwasiliana na serikali. Naye amefanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha haki za wanawake zinapatiwa kipaumbele Somalia.”

Bwana Nyanduga alianza jukumu lake hilo mwezi Juni mwaka 2014.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter