Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa sasa hakuna visa vya Ebola nje ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo-WHO

Wahudumu wa afya wakipuliziwa dawa kama njia ya kujikinga dhidi ya Ebola baada ya kutoa matibabu huko Beni, DRC. (31  Mei 2019)
Finnish Red Cross/Maria Santto
Wahudumu wa afya wakipuliziwa dawa kama njia ya kujikinga dhidi ya Ebola baada ya kutoa matibabu huko Beni, DRC. (31 Mei 2019)

Kwa sasa hakuna visa vya Ebola nje ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo-WHO

Afya

Taarifa ya kila wiki kuhusu Ebola inayotolewa na shirika la afya duniani WHO, imesema kwa sasa hakuna kisa chochote cha Ebola nje ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC. Hata hivyo taarifa hiyo iliyochapishwa hii leo katika ukurasa wa WHO imeeleza kuwa mlipuko wa Ebola unaendelea katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Ituri nchini DRC.

Tangu ripoti ya mwisho ya hali ilivyo kuhusu Ebola, iliyotolewa tarehe 14 Julai mwaka huu wa 2018, visa vipya 91 vimethibitika, wakati huo huo vifo 75 vikiripotiwa kutokea katika majimbo hayo mawili yaliyoathirika.

“Tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya maambukizi, idadi kubwa ya visa ikiwa katika eneo la Beni. Kwa nyongeza, maambukizi yanaendelea kuhamishwa kutoka Beni kwenda katika maeneo mengine kupitia kuhama kwa watu na wale wanaokutana nao.” Imesema sehemu ya taarifa hiyo ya WHO.

Ufuatiliaji wa kina unaendelea kufanywa kwa wale waliokutana na kisa kilichothibitika cha mgonjwa aliyefika Goma tarehe 14 Julai mwaka huu na kuendelea. Wahudumu 19 wa afya walitumwa kutoka katika vituo vingine kwenda Goma ili kutoa msaada kutokana na kisa hiki.

Uvumi kuhusu watu wenye Ebola kusafiri kwenda Bukavu na Kivu kusini, umechunguzwa na kutolewa maamuzi na timu ya ufuatiliaji.

Kiujumla visa vya Ebola vimebakia bila mabadiliko makubwa katika wiki iliyopita. Katika siku 21 kwenye vituo vya afya 65 katika maeneo 18 viliripoti visa vipya asilimia 16 za maeneo 664 zikiwa ni za kutoka Kivu kaskazini na Ituri. Katika kipindi hiki, jumla ya visa 254 vilivyothibitishwa viliripotiwa , wengi wao wakiwa ni asilimia 52 ambayo ni watu 133, Mabalako asilimia 11 yaani watu 28, Madima watu 22 sawa na asilimia 9 na Katwa asilimia 7 sawa na watu 18, maeneo hayo yakiwa ndiyo yameendelea kuwa na milipuko.

Benki ya Dunia nayo yaingilia kati

Hii leo Julai 24, 2019 Benki ya Dunia mjini Washngton Marekani imetangaza kuwa inakusanya fedha kufikia dola za kimarekani milioni 300 ili kuongeza nguvu katika mapambano ya ulimwengu dhidi ya Ebola  nchini DR Congo.

Tangazo hilo linafuatia tamko la WHO kwamba mlipuko wa Ebora wa kipindi hiki ni dharura ya kiafya ya ulimwengu na inastahili kuangaliwa kimataifa.

"Kwa pamoja wote tunapaswa kuchukua hatua ya haraka kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao unateketeza maisha na ustawi wa DRC,” ameeleza Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya dunia Kristalina Georgieva akiongeza, “jamii na wahudumu wa afya waliko katika mstari wa mbele ya kukabiliana na mlipuko huu, wanahitaji msaada zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ili kudhibiti janga lisiwe baya zaidi na pia kujiandaa kupunguza hatari ya kusambaa nje ya mipaka ya DRC.”

Ufadhili huu wa  dola milioni 300 ni msaada na pia mikopo ambayo itapatikana kupitia taasisi ya maendeleo ya kimataifa iliyoko chini ya Benki ya dunia na kiwango hicho ni nyongeza katika dola milioni 100 zlizotolewa na benki ya dunia  tangu mwaka 2018.