Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna ongezeko la maambukizi ya Ebola DRC-WHO.

Wafanyakazi wa WHO kitengo cha kupambana na Ebola wakifika eneo la Komanda, Jimbo la Ituri mashariki mwa DRC, Januari 2019.
WHO/Lindsay Mackenzie
Wafanyakazi wa WHO kitengo cha kupambana na Ebola wakifika eneo la Komanda, Jimbo la Ituri mashariki mwa DRC, Januari 2019.

Kuna ongezeko la maambukizi ya Ebola DRC-WHO.

Afya

Shirika la Afya duniani WHO limetoa ripoti katika tovuti yake ikisema wiki hii kumeshuhudiwa ongezeko la maambukizi ya mlipuko wa Ebola unaoendelea nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC katika eneo la Kivu Kaskazini na Ituri. Katika kipindi hiki vikundi vya wataalamu wa kudhibiti Ebola vinakabiliana na changamoto za kila siku katika kuhakikisha utambuzi kwa wakati na ufuatiliaji wa maambukizi yote katikati mwa vurugu za makundi yenye silaha na pia kutoaminiana miongoni mwa jamii zilizoathirika.

Hata hivyo WHO inasema hatua zimepigwa katika maeneo kama Mandima, Masereka na Vuhovi ambako taratibu timu za watalaamu waliko huko zimeweza kwa mara nyingine na kwa kukubalika na jamii kukata mnyororo wa maambukizi.

Taarifa ya WHO inaeleza kuwa katika siku 21 zilizopita yaaani kuanzia tarehe 6 hadi 26 ya mwezi huu wa Machi, jumla ya visa 125 vya maambukizi mapya vimeripotiwa kutoka katika vituo 51 ndani ya maeneo 12 kati ya 21 yaliyoathirika hadi sasa. 

Asilimia 38 ya maeneo 133 yaliyochini ya uangalizi imeathirika. Idadi kubwa ya walioathirika wanatoka katika maeneo ya Katwa (36), Butembo (14), Mandima (19), Masereka (18) na Vuhovi (17).

Hadi kufikia Machi 26, jumla ya visa 1029 vilivyothibitika na visivyothibitika, vimeripotiwa ambapo kati ya watu hao, 642 wamepoteza maisha. Kati ya visa 1029 vilivyoripotiwa, asilimia 57 yaani watu 584 walikuwa wanawake na asilimia 30 yaani watu 307 walikuwa watoto chini ya umi wa miaka 18.

Idadi ya wahudumu wa afya walioathirika imepanda hadi kufikia 78 sawa na asilimia 8 ya maambukizi, vikiwemo vifo 27.