Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Japo kidogo, mgao wa fedha wasubiriwa kama mlo wa mchana au jioni”- Mnufaika wa ECT

Mwananchi wa Yemen akisukuma mkokoteni wenye chakula cha msaada huko kwenye mji mkuu Sana'a. Mapigano yamesababisha raia wengi kutegemea chakula cha msaada (3 February 3019)
WFP/Annabel Symington
Mwananchi wa Yemen akisukuma mkokoteni wenye chakula cha msaada huko kwenye mji mkuu Sana'a. Mapigano yamesababisha raia wengi kutegemea chakula cha msaada (3 February 3019)

“Japo kidogo, mgao wa fedha wasubiriwa kama mlo wa mchana au jioni”- Mnufaika wa ECT

Msaada wa Kibinadamu

Mzozo wa Yemen ukiingia mwaka wa 5, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema tarkibani watu milioni 9 wamenufaika na mzunguko wake wa 5 wa kuwapatia watu fedha za kujinunulia mahitaji muhimu.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa Yemen, Sana’a imesema kuwa mradi huo wa mgao wa fedha za dharura, ECT usio na masharti, ulianza mwezi Agosti mwaka 2017 ukilenga familia milioni 1.5 zilizo hatarini zaidi.

“Fedha hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa familia ambazo hivi sasa zinakabiliwa na hali ngumu ya uchumi,” imesema UNICEF ikiongeza kuwa familia hutumia fedha hizo kununua vyakula, kulipia huduma za afya, elimu na mahitaji mengine ya msingi.

Mgao wa 5 ulifanyika kati ya tarehe 16 mwezi uliopita wa Juni na tarehe 15 mwezi huu wa Julai ambapo kila familia inapata dola 30 kila baada ya miezi mitatu.

Mmoja wa wanufaika ni Fatima Al-Tayari mjane mwenye umri wa miaka 55 na mkazi wa viunga vya Sana’a ambaye amesema, “fedha ninazopata ninatumia kununua sukari, mafuta na vyakula vingine. Ijapokuwa kiwango si kikubwa, lakini bado kinasaidia kukidhi mahitaji muhimu. Huwa tunasubiri kwa hamu fedha hizi kama vile mtu unavyosubiri mlo wa mchana au wa jioni.”

Benki ya Dunia kupitia wadau wake DFID, serikali ya Marekani inafadhilia mradi huo wa ECT ambapo fedha hupitishwa kwenye taasisi tanzu ya benki hiyo, IDA.

Nchini Yemeni hivi sasa, familia nyingi zimetindikiwa vyanzo vya mapato na ili kuweza kuishi, familia nyingine zimeamua kuchukua hatua za kusikitisha ikiwemo kuoza mapema watoto wao huku watoto wengine wakitumikishwa.

UNICEF inasema vita vikiendelea, watoto nao wanapigana vita vyao wenyewe ikisema kuwa, “usaidizi wa dharura wa fedha unasaidia kulinda familia lakini bado fedha zaidi na msaada zaidi unahitajika kuweza kuzikamua familia hizo.”

Kwa mantiki hiyo UNICEF inasema ili kupunguza machungu ya watoto, “kwanza lazima vita vikome ili ukwamuaji wa uchumi urejee sambamba na maisha ya kawaida. Na wakati huo huo, jamii ya kimataifa iendelee kuipatia Yemen rasilimali zinazohitajika ili kukidhi mahitaij ya watoto katika sekta zote.”