WFP inapambana kurejesha hali nzuri baada ya mafuriko katika kambi za wakimbizi Bangladesh- Herve Verhoosel

23 Julai 2019

Upepo mkali wa monsuni umeendelea kuleta mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko kusambaa na kuleta uharibifu kaskazini magharibi mwa Bangladesh na pia katika kambi ya wakimbizi ya Cox’s Bazar, ameeleza hii leo msemaji mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, Herve Verhoosel.

Verhoosel ameeleza kuwa WFP imewasaidia zaidi ya wakimbizi 11,000 walioathiriwa na mvua na mafuriko kwa kuwaongezea msaada wa chakula zaidi katika wiki mbili za mwanzo za mwezi huu wa Julai.

“Hii ni idadi kubwa zaidi ikilinganishwa na watu tuliowasaidia mwaka 2018.” Ameeleza Bwana Verhoosel.

Kambi za wakimbizi zimeathirika na mamia ya maporomoko ya udongo yaliyotokea nchini humo Bangladesh. Wahandisi wa WFP wamekuwa katika mbio za kuhakikisha wanarejesha hali kwa kuimarisha sehemu za miinuko na mabonde na kutengeneza mifumo ya kupitisha maji ili kupunguza madhara.

Aidha Verhoosel ameeleza kwa matumaini kuwa WFP imejiandaa vema kukabiliana na pepo za monsuni na   imetenga hifadhi ya chakula katika maeneo ya kimkakati karibu na kambi ili kuweza kusambazwa kwa haraka.

“Kazi zimekuwa zikiendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja na kambi zote ziko salama kuliko zilivyokuwa awali.” ameeleza msemaji huyo wa WFP lakini akaongeza kueleza kuwa hivi sasa wako katika nusu ya msimu wa monsuni kwa hivyo msaada kutoka jumuiya ya kimataifa unahitajika ili kuhakikisha kazi liyofanyika katika kambi za wakimbizi inaendelezwa.

Awali kabla ya mvua kubwa na pepo za monsuni kuikumba Bangladesh, tayari WFP kwa kutumia utabiri wa hali ya hewa ilikuwa imetangulia katika eneo hilo na kutoa msaada kwa familia ambazo zilikuwa hatarini.

Takribani familia 5,000 (watu 25,000) katika wilaya ya Kurigram walipokea dola 53 kila familia kwa njia ya kielectroniki. Fedha hiyo imewasaidia watu kulipia mahitaji ya msingi kama vile chakula na huduma nyingine muhimu. 

Msaada huo ulizilenga familia zilizoko hatarini zaidi mathalani zile zinazoongozwa na wanawake, watu wenye ulemavu, na wazee.

Kwa upande wa msaada wa haraka kutokana na mafuriko, WFP inalenga kuwasaidia zaidi ya watu 250,00 katika wilaya tatu za kaskazini magharibi kwa kuwapatia biskuti ambazo zitawasaidia angalau kwa siku tatu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter