Mito 700 inayokatiza Bangladesh yazidi kuweka hatarini taifa hilo wakati wa pepo za monsuni

19 Julai 2019

Nchini Bangladesh, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linafuatilia hali halisi kufuatia mvua kubwa za pepo za monsuni ambazo zimesababisha mafuriko na ongezeko la kiwango cha maji kwenye mito.

Msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi Herve Verhoosel amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa hali inazidi kuwa mbaya zaidi kwenye wilaya za Kurigram, Gaibandha na Jamalpur ambako viwango vya maji vinazidi kuongezeka.

“Hivi sasa tunashirikiana na wadau, zikiwemo serikali za mitaa na kwa mujibu wa takwimu mpya za serikali jumla ya watu milioni 2.3 wameathiriwa na mvua hizo kwenye vitongoji 115 vya wilaya 20.” Amesema Bwana Verhoosel.

Pepo za monsuni zimekuwa na madhara makubwa kila wakati kwa Bangladesh, taifa ambalo lina zaidi ya mito 700 na hivyo kuliweka hatarini na mafuriko pindi mvua hizo zinaponyesha.

WFP inasema pamoja na mafuriko, mabadiliko ya tabianchi nayo yamekuwa ‘mwiba’ kwa Bangladesh kwa kuwa theluji katika miliya ya Himalaya inayeyuka kutokana na ongezeko la kiwango cha joto na hivyo maji ya mito yanatiririka kuelekea taifa hilo.

Bwana Verhoosel ametolea mfano wa wakazi wa wilaya ya Kurigram akisema wao wako hatarini zaidi kwa sababu eneo lao lipo katika kingo za mito. “Pindi kuna mafuriko, nyumba zao na ardhi yao ya mashamba na mbinu zao za kujipatia kipato vinasombwa,” amesema msemaji huyo wa WFP.

Kwa mantiki hiyo amesema ndio maana kwa miongo kadhaa sasa WFP inakuwa mstari wa mbele kuwajengea mnepo wakazi wa nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni 161 ili waweze kukabiliana na majanga  hayo.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter