Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki Afrika na mbinu za kuleta utangamano kati ya vijana na polisi nchini Kenya

Mahojiano na Wevyn Muganda, Meneja Programu wa Haki Afrika
UN News/Assumpta Massoi
Mahojiano na Wevyn Muganda, Meneja Programu wa Haki Afrika

Haki Afrika na mbinu za kuleta utangamano kati ya vijana na polisi nchini Kenya

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Kenya, shirika la kiraia la Haki Afrika limechukua hatua ya kufuata vijana maskani kama njia mojawapo ya kufanikisha utekelezaji wa lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Afisa mradi wa Haki Afrika, Wevyn Muganda amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu amani na usalama na jinsi ya utekelezaji wa ajenda ya vijana na amani.

Bi. Muganda ametaja sababu ya kwenda maskani akieleza kuwa, "maskani  haya ndio mahali ambapo vijana wengi wanaenda kukutana, ni mahali wanajisikia wako huru kuongea yale mambo ambayo wanapenda kusema.  kwa hiyo sisi kama shirika tuliona ni vyema kwenda kwenye haya maeneo ya vijana na kuzungumza nao waweze kutoka katika mawazo ya uhalifu, ama mawazo ambayo kuwa wao wametengwa au hawawezi kuwa watu wenye kazi zao, watu wa kawaida ambao wana heshima zao katika jamii.. Pale kwenye maskani tukienda hatuendi kama shirika, bali tunaenda kama watu katika jamii tunataka kusikia vijana wana maoni gani kuhusu maendeleo, amani, usalama na hata ufisadi. Tukifika pale tunaongea nao hata kama wapo na mogokaa au mirungi, tunawaacha waendelee kwa maana tumewakuta pale. "

Afisa mradi huyo wa Haki Afrika ametoa mfano wa moja ya hatua wanazochukua kuimarisha utangamano kati ya vijana na vyombo vya dola akisema kuwa, " lazima tuwavutie, lazima tufahamu wanapenda nini, kuna wengine tunawapeleka pikniki, tunaona kuwa huyu labda yuko na shida na polisi, kwa hiyo kama tunataka kuleta utangamano kwenye jamii, lazima polisi na vijana waelewane. Kwa hiyo tunaweza kuwapeleka bustani  tuone wanyama, tunachukua polisi. Wale polisi ambao tunafahamu kuwa wanapenda kukwaruzana na vijana, tunawa chukua na wale vijana, tunawapeleka, wanakaa chini na wanaongea. Lakini si hivi hivi lazima kwanza tuwaweke kwenye mazingira ya kutulia na hadi wanasahau kuwa wao ni polisi, baada ya hapo wanaanza kukaa pamoja na kusikilizana na ndipo tunachukua fursa kuwauliza shida iko wapi."  

Lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu linapigia chepuo masuala ya haki, utawala bora na taasisi thabiti.