Blogu ya Beyond the Lines yawezesha vijana kuelewa SDG 16

29 Julai 2019

Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya ambaye pia ni afisa programu wa shirika la kiraia la Haki Afrika Wevyn Muganda amezungumzia vile ambavyo blogu yake ya Beyond the Lines inasaidia kuwezesha vijana kusoma taarifa mbalimbali bila ugumu wowote na hivyo kufanikisha leng namba 16 la maendeleo endelevu, SDGs kuhusu amani,  haki na taasisi thabiti.

Bi. Muganda alizungumzia blogu hiyo hivi karibuni wakati alipohojiwa na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ya ajenda ya vijana katika ufanikishaji wa amani duniani.

Mwanaharakati huyo amesema kuwa, "Ukienda katika Beyond the Lines, lugha inayotumika hapo ni rahisi sana, si lugha ya katiba au ya mawakili, ni lugha  ambayo mtu yeyote anaweza kusoma na kuelewa. Na pia ukitaka kusoma sayansi ya usalama, pia kuna maktaba ambayo unaweza ukapakua na ukasoma. Hii ni kwa mtu ambaye amesoma makala na ana hamu ya kufahamu zaidi au anataka awe mtaalamu ili aweze kusaidia wengine. Sasa basi kuna makala pale imefanywa na wataalamu wengine, si mimi. Nimeweka pale  ili wengine waweze kuzipata kwa urahisi."

Bi. Muganda amasema Beyond the Lines ilianza mwaka 2017 na kwamba aliona kuna changamoto hata kwa wafanyakazi wenzake katika Haki Afrika akisema kuwa, "Kuna taswira ya kwamba kusoma kunachosha na wengine wanasema ukitaka kuficha fedha ifiche  kwenye kitabu, lakini ukiweka kwa simu si rahisi. Kwa hiyo tukasema kuwa ni kwa jinsi gani tunatoa hii elimu kwenye kitabu na tuweke pale mahali vijana wanapenda. Ni muhimu sana twende pale vijana wanapenda. Kama si hivyo basi vitu ambavyo tunafanya havitakuwa na manufaa tunatarajia."

Blogu hiyo ni www.beyondthelines.org

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter