Vijana si waleta vurugu bali ni wajenga amani- Jayathma

17 Julai 2019

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu uendelezaji wa amani na usalama duniani likiangazia zaidi utekelezaji wa ajenda ya vijana na amani.

Akihutubia wajumbe wa Baraza hilo, Mjumbe Maalum wa Katibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake ameangazia hali ya sasa na mwelekeo ili hatimaye vijana wawe washiriki thabiti na si watazamaji wa amani na usalama duniani.

Bi. Wickramanayake ameeleza bayana licha ya fikra potofu ya kwamba vijana ni waleta fujo, ukweli ni kwamba vijana hivi sasa, wanaandamana, wanajipanga na kutekeleza harakati zao za kujenga amani kwenye jamii na mataifa yao.

Amesema  kuwa, “hivi sasa vijana hawasubiri kualikwa kwenye meza za mazungumzo, bali wanasonga na kuwasilisha suluhu mbadala za kutatua matatizo yanayowahusu.”

Ametolea mfano huko Cameroon ambako amesema chini ya uongozi wa vijana wajenga amani, wasuluhishi vijana 600 wamepatiwa mafunzo ya kuweza kuchagiza mashauriano katika ngazi ya jamii zao.

Halikadhalika amegusia tukio la wiki iliyopita huko Libya, ambako vijana 30 kutoka jamii za wachache kutoka Amazigh, Tabu na Tuareg, ikiwemo watu wenye ulemavu ambao walikusanywa na kujadili hoja kuhusu amani, watu, ustawi, sayari na ubia.

Bado vijana wanakumbwa na vitisho

Hata hivyo amesema licha ya harakati hizo za vijana ambazo amezishuhudia wakati wa ziara zake kuanzia Ulaya, Afrika, Asia hadi Amerika, jambo moja linamtia hofu ambalo ni “katika miezi iliyopita nimeona jambo moja linalotia hofu, matukio ya vijana wajenga amani na watetezi vijana wa haki za binadamu kukabiliwa na vitisho, kukamatwa kiholela na kufanyiwa visasi na vikundi vya kiserikali na visivyo vya kiserikali.”

Bi. Wickramanayake amekumbusha kuwa ulinzi ni msingi wa azimio namba 2250 na kwamba “natoa wito kwa serikali kuzingatia na kulinda haki za msingi za vijana, ikiwemo uhuru wao wa kujieleza iwe kwenye mitandao ya kijamii au nje ya mitandao hiyo.”

UN/Evan Schneider
Wevyn Muganda, kutoka shirika la kiraia la Haki Afrika nchini Kenya akihutubia Baraza la Usalama wakati wa mkutano kuhusu amani na usalama hususan ajenda ya vijana na amani.

Haki Afrika na umuhimu wa maskani ya vijana

Mtoa hotuba mwingine kwenye mkutano huo alikuwa Wevyn Muganda, Mkurugenzi kutoka Haki Afrika, shirika la kiraia lenye makao yake makuu huko Mombasa nchini Kenya likihusika na masuala ya haki za binadamu na maendeleo hususan wanawake na vijana na kukabiliana na fikra potofu kuhusu misimamo mikali.

Hakuna amani bila haki,” amesema Bi. Muganda kwenye hotuba yake akisema kuwa “ndio maana tunashirikiana na ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Kenya kusaka haki ya watu 136 waliopotea kwenye pwani ya Kenya tangu mwaka 2012 hadi leo hii, wengi wao wakiwa vijana.”

Ametaja masuala mengine wanayoshughulikia kuwa ni kile alichokiita, “ghasia ya kuenguliwa ambapo vijana wanaonekana kama manusura wa hali iliyopo na pia wachochezi wa ghasia na si washiriki.”

Amesema changamoto kubwa hivi sasa ni jinsi ya kuwaleta vijana kushirikiana nao wakitambua kuwa vijana si wafanya ghasia.

Bi. Muganda ametaja mkakati anaofanya kujumuisha vijana kuwa ni kukutana nao kila Jumapili ambapo huwatembelea maskani ili kusikiliza madhila yao.

“Ingawa tafiti zinaonesha kuwa polisi mara kwa mara huenda maskani kubughudhi vijana kwa madai kuwa ndipo wanatumikishwa kwenye ugaidi, ni huko maskani ambako tumepata washiriki wengi kwenye mafunzo ya haki, ujenzi wa amani na uongozi,” amesema Bi. Muganda akiongeza kuwa vijana hao wanashiriki katika ulinzi jamii au sungusungu.

Halikadhalika ametaja mbinu nyingine za mtandaoni za kufikia vijana katika masuala ya amani akisema kwenye mtandao ana ukurasa uitwao Beyond the Lines ambako “ninachapisha simulizi chanya kuhusu vijana na mbinu za kujumuisha vijana kwa lengo la kuwa na jamii ya mtandaoni ya wajenga amani.”

Ametaja pia mtandao wa Kauli zetu Mtaani, ambamo kwao huchapisha video zenye simulizi za vijana kutoka maskani akisema kuwa, “kila sauti lazima isikike na tutoke mijini na kwenye maofisi hebu na tuende kwenye maskani tukutane na vijana."

UN/Kweku Obeng
Mjumbe maalum wa UN kwa vijana Jayathma Wickramanayake (aliyevalia nguo ya njano) akikutana na wasichana huko Ghana mwezi Februari mwaka 2018

Utekelezaji wa maazimio 2250 na 2419

Kwa mujibu wa Bi. Wickramanayake, mwezi Machi mwakani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atawasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ripoti yake kuhusu vijana na amani na usalama kwa mujibu wa mazimio namba 2250 na namba 2419 ya  baraza hilo.

Azimio 2250  lilipitishwa mwezi Disemba mwaka 2015 ambapo pamoja na mambo mengine lilisihi nchi wanachama kuwapatia vijana mazingira bora ya kutekeleza harakati za kukabiliana na ghasia kwenye maeneo yao na pia ujenzi wa amani sambamba na kufanya utafiti kuhusu vijana, amani na usalama.

Utafiti huo ulikuwa msingi wa azimio la pili namba 2419 lililopitishwa tarehe 6 mwezi Juni mwaka 2018.

Azimio namba 2419 linatambua mchango wa vijana katika kuzuia mizozo na lilimtaka Katibu Mkuu awasilishe ripoti ya utekelekezaji wa maazimio hayo mawili 2419 na 2250 kabla ya mwezi  Mei mwaka 2020.

 

TAGS: Wevyn Muganda, Haki Afrika, Jayathma Wickramanayake

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud