Matarajio yetu kwa dunia iliyo sawa ni kwenu vijana: Guterres

Tukio la kuzindua  mkakati wa vijana wa Youth2030 wa Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Mark Garten)
Tukio la kuzindua mkakati wa vijana wa Youth2030 wa Umoja wa Mataifa.

Matarajio yetu kwa dunia iliyo sawa ni kwenu vijana: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa leo umezindua mkakati wake mpya wa kuimarisha mchango wa takribani vijana bilioni 2 duniani  kwa lengo kukuza amani, uadilifu pamoja na kuwa na  dunia endelevu.

Akizindua mkakati huo hii leo, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, “matarajio yetu yote ya kuwa na dunia nzuri yanawategemea vijana. Maendeleo endelevu, haki za binadamu,pamoja na amani usalama vyaweza tu kupatikana  ikiwa tutawawezesha vijana hawa kama viongozi na kuwawezesha kutumia kikamilifu uwezo wao.”

 Mkakati huo mpya umepatiwa jina la,  “Vijana 2030:Mkakati wa  Umoja wa Mataifa  kwa vijana,”  na uzinduzi umeshuhudiwa siyo tu na vijana wenyewe bali pia viongozi na wakuu wa nchi akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Umoja wa Mataifa unasema licha ya kuwa kizazi cha sasa ndicho chenye idadi kubwa zaidi ya vijana kuliko makundi mengine sambamba na kuwa na teknolojia za hali ya juu, bado kinakumbana na changamoto nyingi.

“Wengi hawapati elimu bora na hupata taabu kupata ajira nzuri. Isitoshe hawana huduma safi ya kiafya pamoja na kuhusu masuala ya kujamiiana na vilevile afya ya uzazi. Kuna nafasi chache ambazo wanaweza kushiriki kuamua mustakhbali wao,” imesema ripoti kutoka ofisi ya mjumbe wa vijana wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Mkakati mpya  unataka kuimarisha  na kuongeza  azma katika ngazi zote , kimataifa, kikanda na kitaifa ili kushughulikia mahitaji ya vijana na kuwapa haki zao na kutambua mchango wao kama chombo cha kuleta mageuzi. “Mkakati huu unatilia mkazo umuhimu wa kuwahusisha vijana ili wachangie kikamilifu kazi za Umoja wa Mataifa na kuhakikisha kuwa  Umoja wa Mataifa unafaidika na ushauri pamoja na mawazo yao,” imesema taarifa hiyo.

Naye mjumbe wa Katibu Mkuu kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake,  amesema kuwa huu ndio mwanzo wa  mwelekeo mpya wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa  vijana sio tu wanasikika lakini pia wanaeleweka na kuwezeshwa  katika ngazi zote  ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.