Tuko tayari kusaidia Marekani kukabiliana na suala la wasaka hifadhi- UNHCR

16 Julai 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeelezea wasiwasi wake kufuatia masharti mapya yaliyotolewa na Marekani kwa watu wanaotaka kusaka hifadhi nchini humo.

Kanuni hiyo mpya iliyotolewa na serikali ya Marekani inataka watu wanaofika mpaka wa kusini na Marekani lazima wawe wamewasilisha maombi yao ya kusaka hifadhi Marekani wakiwa nchi ya tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa UNHCR Liz Throssell amesema, “wakati UNHCR inatambua kuwa mfumo wa Marekani kwa wasaka hifadhi umezidiwa uzito, bado shirika hili liko tayari kushirikiana ili kusaka ahueni na kwamba hatua ya sasa inahatarisha maisha ya watu na familia zilizo hatarini zaidi.”

Bi. Throssell amesema hatua hizo pia zinakandamizi  harakati za pamoja zinazofanyika kwenye ukanda wa Amerika wa kushughulikia watu wanaohama kutoka nchi za kaskazini mwa Amerika ya Kati kuelekea Marekani.

Ameongeza kuwa, “kanuni hii ya mpito kwa kiasi kikubwa inadhibiti haki ya mtu kuomba hifadhi. Tunafikiri kuwa inakwamisha haki ya ulinzi na inaongeza mzigo kwa wasaka hifadhi wa kutaka kujithibitisha na ni zaidi ya viwango vya kimataifa.”

Halikadhalika amesema kanuni hiyo mpya inapunguza haki ya msingi na uhuru wa wale walioweza kufikia uwezo wa kujithibisha lakini haiendani na wajibu wa kimataifa.

Ni kwa mantiki hiyo, UNHCR imetoa wito kwa serikali zote kwenye ukanda wa Amerika ya Kati kushirikiana ili kusaidia idadi kubwa ya watu wanaoondoka eneo la America ya Kati

“Mfumo wa uhakika  unahitajika sambamba na mazingira bora ya mapokezi katika nchi mbalimbali. UNHCR inashirikiana na mamlaka za Guatemala na Mexico ili kufanikisha mpango huo,” amesema Bi. Throssell.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud