Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yasaidia wahamiaji walioko kwenye msafara wa watu Amerika ya Kusini

Msafara wa  kwanza wa wahamiaji walioko kwenye miguu umefika mji wa Matías Romero katika mkoa wa Oaxaca Novemba 1. Wizara ya mashauri ya kigeni ya Mexico inakadiria kuwa watu 4,000 walilala hapo.
IOM / Rafael Rodríguez
Msafara wa kwanza wa wahamiaji walioko kwenye miguu umefika mji wa Matías Romero katika mkoa wa Oaxaca Novemba 1. Wizara ya mashauri ya kigeni ya Mexico inakadiria kuwa watu 4,000 walilala hapo.

IOM yasaidia wahamiaji walioko kwenye msafara wa watu Amerika ya Kusini

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji -IOM linaendelea kusaidia wahamiaji walioko kwenye msafara wa miguu huko Amerika ya Kati ambao wameamua kusaka hifadhi Mexico au wanataka kurejea makwao.

Taarifa ya IOM iliyotolewa kwenye ofisi yake ya kanda huko San Jose Costa Rica inasema wahamiaji hao 1500 kutoka katika msafara huo wa wanaosaka hifadhi Mexico wanapatiwa chakula na vifaa mbalimbali  vya kujisafi.

Mkuu wa ofisi ya IOM nchini Mexico,Christopher Gascon, amesema kuwa ,IOM bado inashikilia msimamo wake kuwa haki za binadamu na mahitaji yote ya msingi wahamiaji lazima yaheshimuwa bila kujali hadhi yao ya  uhamiaji.

 Amesema “ kwa ushirikiano na UNHCR tunaendelea kufuatilia  hali halisi ya msafara huo wa watu tukitegemea mno taarifa kutoka kwa maafisa wetu walioko huko mashinani na ofisi ya kusaidia wahamiaji na wakimbizi ya Mexico-DAPMvR pamoja na asasi zingine ambazo zinawasaidia kwa kuwapatia taarifa kuhusu njia mbadala na salama za uhamiaji na pia nafasi ya kurejea nyumbani kwa hiari.”

Msafara wa pili wenye watu wanaokadiriwa kufikia 1,800, wote wakiwa wahamiaji kutoka nchi za Amerika ya kati waliokubaliwa  na maafisa wa uhamiaji wa Mexico siku ya jumatatu, uliwasili katika mji wa Huixtla, mkoa wa Chiapas  juzi jumatano na unapanga kuanza  tena safari yao leo, kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo.

Kundi hilo mwanzo lilikuwa limeanza utaratibu wa kuruhusiwa kubakia Mexico kihalali  kama wakimbizi lakini tena likaamua kusonga mbele hadi sehemu za kaskazini mwa mpaka.

Msafara wa tatu, wa wahamiaji 500, uliondoka El Salvador jumapili iliyopita na kuvuka mpaka  hadi Mexico Jumanne ya wiki hii ambapo idadi kubwa ya walioko kwenyemsafara huo waliomba hifadhi Mexico.

Kundi la nne la watu 1,700 liliondoka San Salvador Oktoba 30 ambapo msafara wa mwisho ulilala Tecun Uman, mji wa Guatemala  ulioko mpakani na Mexico.