Kwa raia wa Honduras, nyumbani kuchungu, kusaka hifadhi ugenini shubiri

22 Agosti 2018

Umasikini , unyanyasaji na utekaji nyara kutoka magenge ya uhalifu ni kichocheo kwa raia wengi kutoroka nchi zao huko kusini mwa  bara la Amerika , na kusaka maisha bora Marekani. 

Eric kijana mwenye umri wa miaka 17 kutoka kijiji cha Progreso, nchini Honduras ni miongoni mwa wasaka hifadhi waliofunga safari ya kwenda kusaka maisha bora Marekani.

Kwa uchungu Eric anaeleza kilichosababisha yeye na familia yake kukimbia Honduras .

“Siwezi kusema kuwa nimefurahia utoto wangu. Mwanzoni nilihisi kuwa na majukumu zaidi ya umri wangu. Nilihisikuwa na mzigo mkubwa. Wakati mwingine nilimsikia mama yangu akilia, kwa sababu alishindwa kutuhudumia kwa kuwa alikuwa hana pesa wala kazi.”

Akiwa na umri wa miaka 9, yeye, mama yake pamoja na mdogo wake wa kike waliwekwa korokoroni nchini Mexico wakati wakijaribu kuingia Marekani  na baadaye kurudishwa Honduras .

UNICEF/Tanya Bindra
Mama akitokwa machozi akisubiri kukutana na mtoto wake wa kiume ambae amerejeshwa kwa nguvu kutoka Mexico.

“Baada ya miezi minne korokoroni tulirudishwa Honduras tukiwa hatuna chochote.”

Sasa ni miaka minane tangu Erik na familia yake warudishwe kutoka Mexico, bado wanaendelea kuishi maisha ya kutokuwa  na uhakika na vilevile  hawana fedha za kuendelea kulipia kodi ya  nyumba wanamoishi.

“Ningependa sana kumsaidia mama yangu mzazi, kwa sababu nahisi anastahili.”

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imebaini kuwa asilimia 70 ya watoto nchini Honduras wanaishi katika umasikini uliopindukia.

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter