Manusura wa boti iliyozama Mediteranea waelezea safari yao ilivyokuwa

5 Julai 2019

Zaidi ya wahamiaji 80, miongoni mwao wanawake na watoto yasadikiwa kuwa walizama wiki hii baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama kwenye bahari ya Mediteranea, nje kidogo ya pwani ya Tunisia. 

Mkuu wa ofisi ya shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM nchini Libya, Lorena Lando amesema kupitia taarifa  iliyotolewa leo mjini Zarzis nchini Tunisia, kuwa jana Alhamisi walisaidia manusura wanne wanaume ambao walieleza kuwa walisafiri kwa boti kutoka Zwara nchini Libya mapema jumatatu wiki hii.

Miongoni mwao alikuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 29, raia wa Côte d'Ivoire ambaye alifariki dunia mapema jana baada ya mwili wake kushindwa kustahimili baridi.

Wakielezea safari yao, manusura hao wamesema kuwa boti lao la kujazwa upepo lilikuwa limebeba watu 86 wakiwemo wanawake wanne na watoto wawili na liliondoka Zwara majira ya saa 12 asubuhi ya tarehe mosi mwezi huu.

Wameeleza kuwa saa chache baadaye, boti yao ilianza kuingia maji na purukushani za abiria zikasababisha chombo hicho kuzama.

IOM inasema saa 40 baada ya kuwemo kwenye maji, wavuvi waliwaona wanaume hao na kupeleka taarifa kwa walinzi wa pwani wa Tunisia ambao waliwaokoa na kuwafikisha eneo la Zarzis.  

Lando amesema kuwa manusura mwingine yuko katika hali nzuri akipatiwa matibabu na hawezi kuhojiwa kwa sasa.

Kwa mujibu wa IOM, hili si janga la kwanza kwa mwaka huu ambapo tarehe 10 na 11 mwezi Mei mwaka huu uokozi ulifanyika kutoka kwa vyombo viwili vya majini viliyokuwa vimejaza abiria kupita kiasi.

Mwaka huu pekee watu 426 wamezama wakijaribu kuvuka Mediteranea, ilihali wengine 3,750 wameokolewa na kurejeshwa kwenye vituo vya kushikilia wahamiaji huko Libya.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter