Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na wahamiaji wanaoshikiliwa Libya lazima waachiliwe huru:UN

Mkuu wa ujumbe wa UNHCR nchini Libya, Jean-Paul Cavalieri, alipowasili katika kizuizi cha Tajoura.
© UNHCR/Mohamed Alalem
Mkuu wa ujumbe wa UNHCR nchini Libya, Jean-Paul Cavalieri, alipowasili katika kizuizi cha Tajoura.

Wakimbizi na wahamiaji wanaoshikiliwa Libya lazima waachiliwe huru:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la uhamiaji IOM, wametoa wito kwa Muungano wa Ulaya EU na Muungano wa afrika AU, kubadilisha mtazamo kwa wakimbizi na wahamiaji nchini Libya na kutekeleza hatua kadhaa zenye lengo la kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji waliokwama kwnye vituo mbalimbali Libya au wanaojaribu kuchukua safari za hatari kwenye bahari ya Mediterranea.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa Alhamisi wiki hii mashirika hayo yamesema kufuatia shambulio la anga la wiki hii kwenye kituo kinachoshikilia wakimbizi na wahamiaji cha Tajoura ambalo lilikatili maisha ya watu 50 katika vituo mbalimbali vya wakimbizi na wahamiaji , mashirika hayo yametoa wito kwa wakimbizi na wahamiaji 5,600 anaoshikiliwa katika vituo mbalimbali nchini Libya kuachiliwa huru na kwa mpangilio ili waruhusiwe kuishi katika jamii au katika vituo ambavyo viko wazi na husu sio kama jela.

Kituo cha Tajoura hivi sasa kimefungwa baada ya shambulio hilo na manusura 400 wamehamishiwa katika kituo cha UNHCR cha ukusanyaji na usafirishaji wa wakimbizi na wahamiaji ili kusubiri kupelekwa mahala pengine.

Taarifa hiyo ya pamoja pia imetoa wito kwa nchi za Muungano wa Ulaya kufufua mpango wa kuwaska na kuwaokoa watu kwenye bahari ya Mediterranea, kuacha kuziadhibu boti za mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuokoa maisha ya watu baharini, na kufikia muafaka wa wapi wakimbizi na wahamiaji waliokolewa washushwe kutoka kwenye boti hizo.

Watu zaidi ya 80 wanasadikiwa kufa maji baada ya kuzama wiki iliyopita baada ya boti yao iliyoondoka mwambao wa Libya kuzama kwenye Pwani ya Tunisia. Shirika la chama cha msalaba mwekundu la Tunisia na walinzi wa Pwani wa nchi hiyo wamesema wameopoa maiti 38 kutoka katika boti hiyo jana Alhamisi.