Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za mabadiliko ya tabianchi Saint Lucia ni fursa ya dunia kushirikiana kukabiliana nazo- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na jamii ya mataifa Caribbea Julai 3 nchini St. Lucia.
Ofisi ya msemaji wa UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na jamii ya mataifa Caribbea Julai 3 nchini St. Lucia.

Athari za mabadiliko ya tabianchi Saint Lucia ni fursa ya dunia kushirikiana kukabiliana nazo- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres yuko ziarani visiwa vya Saint Lucia ambako amekutana na viongozi na wakuu wa serikali katika visiwa hivyo vilivyoko eneo la Carribea.

Bwana Guterres akizungumzia uzuri wa visiwa vya Saint Lucia amesema uzuri na upekee wa visiwa vya Carribea unatishiwa na changamoto zinazokabili mataifa ya visiwa vidogo yanayoendelea ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na vikwazo vingine vinavyotishia ufikiaji wa maendeleo endelevu ikiwemo ulinzi wa raia na kuwajengea mnepo na ufikiaji wa fedha.

Katibu Mkuu huyo amekumbusha ziara yake ya Pasifiki ambako alishuhudia namna mataifa hayo yanakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwekeza kwa ajili ya maendeleo kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.

Guterres ameongeza ni miaka miwili tu tangu aizuru Carribea kushuhudia athari za vimbunga Irman na Maria mwaka 2017 ambapo amesema athari hizo bado zipo katika mawazo ya watu wa Carribea na wakati majanga ya aina hiyo yakiendelea kushuhudiwa hatari kwa familia na maendeleo inaendelea kuongezeka.

Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres ametaja umuhimu wa kupunguza uchafuzi wa mazingira na kufanya kazi pamoja kudhibiti ongezeko la joto duniani na kusalia nyuzi joto 1.5. Hivyo ametolea wito viongozi wa serikali na sekta binafsi kuwasilisha mipango yao katika kongamano la harakati dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kabla ya Disemba 2020 kwa jili ya kupunguza hewa chafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030.

Bwana Guteres ametambua mchango wa mataifa ya visiwa vya Carribea katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hususan kupunguza uchafuzi wa hewa na kubuni kawi endelevu kwa jili ya kuzalisha umeme endelevu.

Uchafuzi wa plastiki

Bwana Guterres ametaja uchafuzi wa plastiki, mmomonyoko wa fukwe za bahari, matukio makubwa ya hali ya hewa, ongezeko la kina cha bahari na kupotea kwa bayoanuai, kama baadhi ya changamoto zinazokabilia mataifa ya Caribbea. Amepongeza mataifa hayo kwa kuwasilisha malengo yake ya kufanya ukanda huo kuwa eneo linalostahimili mabadiliko ya tabianchi. 

Katibu huyo amesisitiza kwamba wanawake wako katikati mwa suala la kujenga mnepo ukanda wa Carribea na kwingineko. Hivyo amepongeza ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Ulaya na mataifa ya Caribbea katika kuwekeza kwa wanawaka na wasichana na kukabiliana na ukatili dhidi ya wasichana na wanawake.

 Changamoto za kiuchumi

Katibu Mkuu katika hotuba yake amesema kando na gharama za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, mataifa ya visiwa vidogo yanayoendelea yanakabiliwa na changamoto za kiuchumi kwa sababu ya soko dogo nyumbani na uwezo mdogo kwa kushiriki soko la kimataifa na kutegemea bidhaa za nje na hivyo kuyaweka mataifa hayo katika hatari ya mfumko wa bei ba deni kubwa la taifa linaongeza viwango vya umaskini na ukosefu wa usawa. 

Ameesma hali ni mbaya zaidi kufuartia changamoto za mataifa hayo kupata mikopo. Kwa mantiki hiyo amesema Umoja wa Mataifa unalenga kufanya mabadiliko ili kuweza kusaidia nchi kufikia malengo ya maendelo endelevu ifikapo 2030.

Ushirikiano na UN

Bwana Guterres amepongeza mataifa ya Carribea kwa ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa na katika kukabilian na changamoto za kimataifa ikiwemo usafirishaji haramu, suala la wakimbizi na wahamiaji.