Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnaosuasua kutekeleza mkataba wa Paris tazameni India- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) akimpatia tuzo Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, tuzo ya bingwa wa mazingira duniani mjini New Delhi, India. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Erik Solheim
UN /Deepak Malik

Tabianchi na mazingira

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameibuka mshindi wa tuzo ya bingwa wa dunia wa kuhifadhi mazingira inayotolewa kila mwaka na Umoja wa Mataifa. Tuzo hiyo amekabidhiwa leo mjini New Delhi, India ambako Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres yuko ziarani. 

Mjini New Delhi, India, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisihi hadhira iliyojumuika naye kumpongeza Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kwa kushinda tuzo hiyo kwa kuzingatia ujasiri na uongozi wake wa kusongesha nchi yake kwenye uchumi usioharibu mazingira.

Miongoni mwa hatua za kisera alizotekeleza Modi ni kutangaza na kuwa India itaondokana na matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja na kutupwa ifikapo mwaka 2022, ikiwa ni uamuzi wa kijasiri wakati huu ambapo baadhi ya viongozi wanasuasua au wanapuuza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi kwa hofu ya kukwamisha maendeleo. “Viongozi wengine wanapaswa kuangalia kile kinachoendelea India na kufanya vivyo hivyo, bila shaka kwa kuzingatia mazingira yao, kuhakikisha tuna uwezo wa kushinda mbio dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Na kwamba tuna uwezo wa kuelewa kuwa hii le hakuna mgogoro kati ya hatua dhidi ya tabianchi na maendeleo.”

Mama na mwanae wakiwa kando mwa jiko lisilohifadhi mazingira ambalo ni shida kwa afya yao.
Benki ya Dunia/Prabir Mallik
Mama na mwanae wakiwa kando mwa jiko lisilohifadhi mazingira ambalo ni shida kwa afya yao.

Na zaidi ya yote ni mbinu bunifu ya kutumia majiko ya ndani ya nishati ya mkaa usiotoa moshi.

“Ukweli ni kwamba kwa kuwa na majiko haya sanifu, India inatatua suala la  uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba ambao unaathiri wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa na ni njia nyingine ya kudhihirisha kuwa uchumi unaojali mazingira na unaostawi," amesema Guterres.

India pia imejikita katika kuzalisha nishati ya jua ambapo Katibu Mkuu amesema ni kutokana na uongozi wake India ni ya tano duniani kwa kuzalisha nishati hiyo na mwelekeo ni kwamba nafasi hiyo inaweza kupanda juu.

Tuzo ya bingwa wa dunia ilianza kutolewa mwaka 2013, ambapo miongoni mwa washindi ni Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye alitunukiwa tuzo hiyo mwaka 2016.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi katika picha hii ya maktaba wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN/Cia Pak
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi katika picha hii ya maktaba wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa