Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi wa UN na wa DRC waanzisha doria za pamoja Butembo

Walinda amani wa MONUSCO nchini Congo DRC, wakifanya doria mjini Butembo Januari 2019.
MONUSCO
Walinda amani wa MONUSCO nchini Congo DRC, wakifanya doria mjini Butembo Januari 2019.

Polisi wa UN na wa DRC waanzisha doria za pamoja Butembo

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, polisi wa Umoja wa Mataifa, UNPOL kwa kushirikiana na jeshi la polisi nchini humo wamezindua doria za pamoja kwenye mji wa Butembo katika jimbo la Kivu Kaskazini kwa lengo la kukabiliana na vikundi vya kihalifu vilivyojihami kwenye eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshansa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, DRC, imesema kuwa vikosi 20 vya polisi wa Umoja wa Mataifa kutoka Senegal na Misri vimeungana na polisi wa DRC ili kuimarisha usalama wa raia.

Wakati wa uzinduzi wa doria hiyo ya pamoja, maafisa kutoka polis iwa DRC wamesisitiza umuhimu wa operesheni hiyo na faida zake katika usalama wa raia kwa kuzingatia kuwa jukumu la kwanza la polisi ni ulinzi wa raia.

Kwa upande wake, Mkuu wa polisi wa Umoja wa Mataifa huko Butembo amesema kuwa, “uzinduzi wa doria hizi za pamoja ni usaidizi wa usalama kwa raia wa Butembo.”

Eneo la Butembo ambako pia ni kitovu cha mlipuko wa Ebola, limekuwa likikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka vikundi vilivyojihami.

Mashambulizi yamekuwa yakilenga vituo vya kutibu Ebola na kusababisha vifo vya siyo tu raia bali pia walinda amani na wahudumu wa afya.