Walimu hawajaandaliwa kufundisha watoto walioathiriwa na vita- UNESCO

20 Juni 2019

Ikiwa leo ni siku ya wakimbizi duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limetaka hatua zaidi kusaidia watoto wakimbizi ambao wanakumbwa na kiwewe pindi wanapokuwa shuleni kujifunza.

Nyaraka mpya ya UNESCO iliyotolewa na kitengo chake cha kufuatilia elimu duniani imesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa idadi ya  watoto wanafunzi waliokumbwa na kiwewe cha vita imeongezeka kwa asilimia 26 tangu mwaka 2000.

Kiwewe hicho kinatokana na vita walivyoshuhudia nyumbani au uzoefu wa kutisha wakati wa safari za kukimbia makwao na hata wakati wa kuanza maisha mapya ugenini, hali ambayo inakwamisha uwezo wao wa kujifunza.

Mfano mmoja ni kutoka Ujerumani kwenye shule moja ya kupokea wageni wakimbizi ambapo mwalimu Jenny Caroline Herbs amesema, “kuna mtoto mmoja mvulana ambaye alishikiliwa korokoroni nchini Iraq, ukimkemea tu, anakimbia na kutoka nje ya darasa na harudi tena. Sikuwa na mafunzo rasmi na ni kweli nazidiwa. Mara nyingi walimu hawatambui watoto wenye kiwewe hawawezi kujifunza kama wattoto wengine. Hawana kimbilio la kutibu kiwewe chao.”

demo%%%Nchini Ujerumani, mtoto 1 kati ya watoto 5 wakimbizi anakumbwa na ugonjwa wa kiwewe baada ya kushuhudia mambo mabaya, PTSD.

UNESCO inasema shule zinasalia kimbilio pekee la kutibu watoto hao kwenye maeneo yasiyokuwa na vituo vya afya.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa kitengo hicho cha GEM Manos Antoninis amesema, “walimu siyo na hawapaswi kuchukuliwa kama wataalamu wa magonjwa ya akili. Lakini wanaweza kuwa chanzo muhimu cha usaidizi kwa watoto wanaougua kiwewe iwapo watapatiwa mafunzo.”

Amesema na kwa kuwa bado mizozo inaendelea ni vyema hatua zikachukuliwa kubadili hali ya sasa ya ufundishaji watoto wakimbizi na wahamaji hivyo UNESCO imewasilisha mapendekezo matano.

Mapendekezo hayo ni pamoja na maeneo ya kujfunzia yawe salama na yajibu mahitaji ya watoto, walimu wanaofundisha wakimbizi na wahamiaji wapatiwe mafunzo sahihi, ushauri wa kisaikolojia unahitajika na utolewe kwa ushirikiano baina ya shule, wataalamu wa afya na wale wa kijamii.

Pendekezo la nne ni kwamba mafunzo hayo ya kijamii na kihisia yazingatie tamaduni za wahusika na tano jamii na wazazi washirikishe katika harakati zote.

TAGS: UNESCO, wakimbizi, wahamiaji, watoto, kiwewe

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter