Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mmoja atapata hasara elimu ya mkimbizi na mhamiaji ikipuuzwa:UNESCO

Watoto wakiwa ndani ya darasa la shule ya hema ya UNICEF katika kambi ya Alhabanya,Anbar, Iraq.Watoto wahamiaji na wakimbizi hukosa elimu wanakokimbilia.
UNICEF/UN0161150/Anmar
Watoto wakiwa ndani ya darasa la shule ya hema ya UNICEF katika kambi ya Alhabanya,Anbar, Iraq.Watoto wahamiaji na wakimbizi hukosa elimu wanakokimbilia.

Kila mmoja atapata hasara elimu ya mkimbizi na mhamiaji ikipuuzwa:UNESCO

Wahamiaji na Wakimbizi

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa ya kufuatilia elimu ikisema idadi ya watoto wahamiaji na wakimbizi duniani waliofikisha  umri wa kwenda shule ikiongezeka na kukaribia kujaza madarasa nusu milioni, Uganda ni miongoni mwa nchi 10 zilizopongezwa kwa kuwapatia wakimbizi fursa sahihi ya elimu.

Ikiangazia wahamiaji na elimu, ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO iliyozinduliwa huko Berlin, Ujerumani imesema na mataifa kama Chad, Ethiopia na Canada, zimejumuisha wakimbizi kwenye mifumo ya elimu ya kitaifa na hivyo kuwa nchi 10 zinazoongoza katika kutekeleza sera jumuishi za elimu kwa wahamiaji na wakimbizi.

Hata hivyo hali ni tofauti kwa wakimbizi wa kabila la Rohingya huko Bangladesh na wa Burundi nchini Tanzania ambako wakimbizi hawapati elimu kupitia mfumo wa kitaifa na hata wanapopata ni kupitia mfumo binafsi ambao baadhi yao hauna ithibati.

Akizungumzia hali ya baadhi ya wakimbizi na wahamiaji kukosa elimu sahihi, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay, amesema “Kila mtu anapata hasara pindi elimu ya wahamiaji na wakimbizi inapopuuzwa. Elimu ni ufunguo wa ujumuishaji na utengamano. Kuongeza utofauti ndani ya darasa, ingawa ni changamoto kwa walimu, kunaweza kuongeza kuheshimiana kutokana na utofauti na pia ni fursa ya kujifunza kutoka kwa wengine. Ni njia bora ya kuimarisha jamii na kuifanya iwe na mnepo.”

Kwa mantiki hiyo ili kuimarisha elimu kwa wahamiaji na wakimbizi, ripoti inatoa mapendekezo  ikiwemo kulinda haki ya wakimbizi na wahamiaji kuelimishwa, kuwajumuisha  wahamiaji na waliopoteza makazi yao katika mifumo ya elimu ya taifa na kuwaandaa walimu wa wahamiaji na wakimbizi  kushughulikia matatizo ya wakimbizi.

Halikadhalika kutumia vizuri, uwezo na vipaji vya wakimbizi na wahamiaji na pia kuunga mkono  mahitaji ya kielimu ya wahamiaji na wakimbizi katika misaada ya kimaendeleo na ya  kibinadamu.

UNHCR imeguswa na ripoti mpya ya UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR hii leo baada ya kuipokea ripoti ya UNESCO kuhusu elimu, limesema uwekezaji zaidi unahitajika.

Naibu Kamishna Mkuu wa  UNHCR  Volker Türk amesema ripoti imekuja wakati muafaka kukumbusha kuwa ahadi ya malengo ya maendeleo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa kuhusu kutomwacha yeyote nyuma yanatakiwa pia kuzihusisha familia na watoto ambao wanakimbia mateso na machafuko.

Türk ameyasema hayo akizungumza wakati wa usomwaji wa ripoti hiyo mjini Berlin Ujerumani na akaongeza kusema kuwa mamilioni ya wakimbizi ambao wanalazimika kuishi uhamishoni kwa miaka mingi, elimu si tu ni njia ya kutatua matatizo ya dunia lakini pia muhimu katika kutatua kisawasawa dharura zozote za wakimbizi. Ripoti hiyo iliyojikita katika wahamiaji na waliokosa makazi imeonesha kuwa zaidi ya nusu ya wakimbizi watoto milioni 7.4 kote duniani wamenyimwa fursa ya elimu.

Türk amenukuliwa akisema, “ katika data zote zilizotolewa, takwimu moja ya wakimbizi inajitokeza zaidi: Hii leo tuna watoto wakimbizi milioni 4 walioko nje ya shule…tunahitaji kufanya zaidi”