Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi Nigeria yasababisha vifo vya watu 30, UN yalaani

Picha ya UN
OCHA/Franck Kuwonu
Picha ya UN

Mashambulizi Nigeria yasababisha vifo vya watu 30, UN yalaani

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mashambulio ya kujilipua huko kijiji cha Konduga kwenye jimbo la Borno, kaskazini- masharibi kwa Nigeria, mashambulio ambayo yamesababisha vifo vya raia.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa katika shambulio hilo la leo mtu mmoja alijilipua kwenye eneo ambako watu walikuwa wanatizama filamu na wengine wawili eneo la jirani ambapo jumla ya watu 30 wameuawa na wengine 40 wamejeruhiwa.

Kikundi cha kigaidi ha Boko Haram kinashukiwa kuhusika na shambulio hilo lakini hadi sasa hakijasema chochote.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Nigeria, pamoja na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

“Hakuna kitu chochote kinaweza kuhalalisha mashambulizi haya na tunasihi mamlaka zichukue hatua haraka ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria,” amesema Bwana Guterres.

Halikadhalika Katibu Mkuu amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Nigeria katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali.

Amerejelea pia ahadi yake kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia harakati za kikanda za kukabiliana na ugaidi.