Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tutambue changamoto za Kaskazini mwa Nigeria ili tuweze kuleta matumaini:Guterres 

Mamia ya maelfu ya watu wamefurushwa kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
UNOCHA/Damilola Onafuwa
Mamia ya maelfu ya watu wamefurushwa kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Lazima tutambue changamoto za Kaskazini mwa Nigeria ili tuweze kuleta matumaini:Guterres 

Amani na Usalama

Changamoto kubwa zinazokabili jimbo la kaskazini mashariki mwa Nigeria la Borno, ambazo ni pamoja na ugaidi, zinahitaji kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa ili kuunda kile ambacho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekiita "hali ya matumaini na hali halisi," katika eneo ambalo amesema halikufikia kilele cha sifa yake ya ugaidi, vurugu, kufurusha watu makwao au kukata tamaa. 

António Guterres ametoa maoni hayo baada ya kutembelea kituo kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa cha kuwajumuisha katyika jamii watoto ambao wamejihusisha na makundi yenye silaha, huko Maiduguri, mji mkuu na mji mkubwa zaidi wa Jimbo la Borno. 

Jimbo la Borno limekuwa moja wapo ya vitovu vya itikadi kali na shughuli za kigaidi nchini Nigeria na katika eneo zima la Sahel. 

Ukosefu wa usalama katika kipindi cha miaka 12 iliyopita unaohusishwa na makundi yenye silaha, likiwemo kundi la kigaidi la Boko Haraam, umeathiri  maisha na kusababisha takriban watu milioni 2.2 kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alitembelea kituo cha huduma ya muda cha Bulumkutu, kilichofunguliwa Juni 2016.  

Kituo hicho kimetoa makazi, ulinzi na huduma nyinginezo za kuokoa maisha kwa watu 7,036, wakiwemo watoto 4,018 (wavulana 2,756 na wasichana 1,262) katika maandalizi ya kurejea kwenye jamii zao. 

Wengi wa watoto hawa walilazimishwa au kuchaguliwa, kwa kukosa fursa nyingine, kujiunga na vikundi vya kigaidi na kuchukua silaha kama wapiganaji. Wengine waliwekwa kizuizini na kisha kuachiliwa baada ya kushukiwa kuhusika na vitendo vya ghasia na machafuko. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipokutana na watoto katika kituo cha muda cha kulinda watoto Maiduguti jimbo la Borno.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipokutana na watoto katika kituo cha muda cha kulinda watoto Maiduguti jimbo la Borno.

 

Baada ya kukutana na kundi la watoto, Bw Guterres amesema: “Nimeshangaa leo kuona katika kituo wale ambao wamekuwa magaidi, wanataka kujumuika na kuchangia katika jamii. Sera iliyopo hapa ni sera ya upatanisho na ujumuishaji upya katika maisha.” 

Migogoro inayoingiliana 

Ugaidi, ghasia na ukosefu wa usalama ambao umeleta madhila kwa jamii sio tu nchini Nigeria lakini pia katika nchi nyingi jirani ni dalili moja ya mchanganyiko wa migogoro inayoingiliana. 

Mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kupungua kwa mvua, kumesababisha mivutano na wakati mwingine migogoro dhidi ya rasilimali chache, ukataji miti na malisho ya mifugo kupita kiasi vimeharibu zaidi mazingira ambayo watu wengi wa kuhamahama wa Sahel wanayategemea ili kuishi na kupelekea wengi wao kuhamia maeneo tofauti, na kuweka shinikizo kwa huduma za msingi ambazo tayari zimelemewa, kama vile afya na elimu. Maelfu ya shule zimelazimika kufungwa, hasa kutokana na ukosefu wa usalama. 

Mahitaji makubwa ya kibinadamu 

Umoja wa Mataifa unasema kuwa mahitaji ya kibinadamu kaskazini-mashariki mwa Nigeria yanaendelea kuwa makubwa, yakichangiwa na janga la COVID-19 na kuzorota kwa hali ya uhakika wa chakula, kutokana na changamoto zinazowakabili wakulima katika kuzalisha na kuuza mazao.  

Takriban watu milioni 8.4 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Kati ya watu hao karibu milioni 3.2 hawapati chakula cha kutosha. 

Mpango wa kukabiliana na misaada ya kibinadamu kwa Nigeria unatoa ombi la dola bilioni 1.1 kusaidia watu hao wenye mahitaji kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo na kwa sasa limefadhiliwa kwa asilimia 8.7 pekee. 

Gharama ya operesheni za kibinadamu imepanda hivi karibuni, kutokana na athari za vita vya Ukraine, huku bei ya dizeli ikiongezeka kwa asilimia 52 kutoka kipindi cha kabla ya mgogoro, nai bei ya mbolea imeongezeka kwa karibu asilimia 49. 

Takriban watu milioni 3.2 hawapati chakula cha kutosha kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
UNOCHA/Damilola Onafuwa
Takriban watu milioni 3.2 hawapati chakula cha kutosha kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

 

Bwana Guterres amesema ni "muhimu kabisa kuelewa kwamba, katika hali kama hii, haitoshi kutoa msaada wa kibinadamu pekee. “ 

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "kuwekeza katika Borno ya matumaini, kutoa msaada kwa miradi ya serikali ya Borno na mashirika ya kiraia ili kuunda mazingira ya maendeleo ya kweli, mazingira ambayo shule zinafanya kazi, hospitali zinafanya kazi na ajira zipo; hali ambayo watu wanaweza kuishi kwa amani na mshikamano.” 

Pia amesema jumuiya ya kimataifa inahitaji kuunga mkono "si tu hali ya matumaini, lakini hali inayostahiki, ambayo hakuna nafasi ya ugaidi."