Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Spika janja aina ya KAYA ni mapinduzi katika teknolojia ya akili bandia- Isaya

Spika Janja, spika ya kwanza kabisa janja kutengenezwa barani Afrika
Smart Kaya
Spika Janja, spika ya kwanza kabisa janja kutengenezwa barani Afrika

Spika janja aina ya KAYA ni mapinduzi katika teknolojia ya akili bandia- Isaya

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kila uchao Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu wake Antonio Guterres unataka matumizi sahihi ya teknolojia hususan ile ya akili bandia au Artificial Intelligence ili kuhakikisha inakuwa na manufaa na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu.

Tayari vijana wameitikia wito huo na miongoni mwao ni Isaya Yunge, kijana mjasiriamali wa teknolojia kutoka Tanzania ambaye ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya teknolojia ya Smart Kaya au Nyumba Janja ambayo imebuni teknolojia kadhaa ikiwemo Spika janja.

Akihojiwa kwa njia ya simu na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Bwana Yunge amesema, “spika janja ni spika ambayo ina uwezo tambuzi karibu na binadamu lakini si sawa na binadamu. Ina uwezo tambuzi wa baadhi ya mambo ambayo imejifunza au kufunzwa kuyatambua na ina uwezo wa kuyajibu au kuyatolea mwongozo sawa sawa na binadamu angeyafanyia lakini yenyewe inakuwa na usahihi zaidi kwenye kutoa majibu hayo. Lakini pili ni ambayo ina uwezo wa kuchukua maelekezo na ikakifanya bila wewe mhusika kufanya kwa mikono yako.”

Alipoulizwa ni kwa vipi spika janja ya Kaya inaleta mapinduzi kwenye teknolojia tofauti na spika janja nyingine Bwana Yunge amesema, “Tanzania kwa mfano ni dhahiri kwamba wagonjwa wa maradhi ya UKIMWI wananyanyapalika, kwa hivyo mara nyingi sana wagonjwa hawa wanakuwa hawana mtu wa kuzungumza naye, wanakuwa hata kupata dawa za kutumia, chakula cha kutumia. Kwa hiyo KAYA inaweza kusaidia vijana wa kiafrika, kwa mfano akiwa nyumbani   moja kwa moja ikamuunganisha na mtaalamu akazungumza naye.”

Bwana Yunge amesema KAYA inasaidia kwa kuwa iwapo kijana anaona aibu kuzungumza na mzazi wake, anaweza akiwa chumbani kwake akazungumza na spika hiyo na kumuelezea kuwa amepima UKIMWI na ana kiwango fulani cha CD4.

Amesema, “KAYA itafika kwenyemfumo wao na kumuunganisha na wataalamu wa afya na akawa na mazungumzo na washauri bila kuonana uso kwa uso. Na hii itakuwa na mashiko zaidi kwa Afrika kwa sababu teknolojia nyingi zinazotoka nchi za Magharibi zinakuwa za anasa zaidi na haziangalii upande wa ubinadamu na utoaji huduma kwa watu.”

Miongoni mwa lugha zitakazokuwemo kwenye spika hiyo ni pamoja na Kiswahili.