Skip to main content

Vyama vya ushirika vyapigwa chepuo

Kilimo bora Afrika ni mojawapo ya nchi za kunufaisha wakulima katika soko la pamoja.
FAO/Olivier Asselin
Kilimo bora Afrika ni mojawapo ya nchi za kunufaisha wakulima katika soko la pamoja.

Vyama vya ushirika vyapigwa chepuo

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha kaya utaanza kuzingatiwa mwakani, hivyo hivi sasa wadau mbalimbali wanachukua hatua ili kilimo kiweze kuwa mkombozi kwa kaya.

Umoja wa Mataifa na shirikisho la kimataifa la vyama vya ushirika, ICA wametia saini makubaliano ya kuendeleza ushirika wao ili kukomboa wakulima wadogo.

Hatua hiyo inayoendeleza ushirikiano kati yao ulioanza  mwaka 2013, inachagiza pia harakati za kuelekea kuanza kwa muongo wa kilimo cha familia au kaya hapo mwakani.

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limesema kupitia makubaliano hayo wakulima wadogo katika nchi zinazoendelea watanufaika na muundo wa kipekee wa kibiashara ambao unajumuisha malengo ya kiuchumi na kijamii ya maendeleo jumuishi.

Mathalani watapatiwa mbinu bora za jinsi vyama vya ushirika katika sekta ya kilimo na chakula vinaweza kuwa endelevu na jumuishi, vyama vinzingatie mahitaji ya wanachama wake na pia kuwekewa mazingira bora ili vyama hivyo vya ushirika vichanue na vistawi.

FAO imesema kila uchao, dunia inaendelea kutambua na kuthamini mchango muhimu wa vyama vya ushirika katika kutokomeza umaskni na kufanikisha upatikanaji wa chakula.

Kwa mantiki hiyo vyama vya ushirika vya kilimo vinavyoendeshwa kidemokrasia na kumilikiwa na wanachama wake ni miundo ambayo inaweza kuendeleza kaya ikafanikiwa kiuchumi, ikafikia soko, ikapata mikopo na hata rasilimali nyingine za kuboresha ustawi wao.

Azimio la kuanzishwa kwa muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha familia linataka kuwekwa msisitizo kwenye vyama vya ushirika vya kilimo na mitandao ya wakulima ili kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe.