Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili Afrika tuzifikie SDGs kwa ubora, inabidi tuanze kukusanya takwimu zetu sisi wenyewe-Isaya Yunge

Isaya Yunge, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa spika janja ya Kaya inayoweza kufanya kazi kwa kumsikiliza binadamu.
UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi
Isaya Yunge, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa spika janja ya Kaya inayoweza kufanya kazi kwa kumsikiliza binadamu.

Ili Afrika tuzifikie SDGs kwa ubora, inabidi tuanze kukusanya takwimu zetu sisi wenyewe-Isaya Yunge

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ili nchi za kiafrika ziweze kufikia kwa ubora malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, inazipasa nchi hizo zibuni teknolojia zao wenyewe zitakazosaidia kukusanya takwimu za kijamii badala ya kutegemea data na mipango kutoka nje.

Ushauri huo umetolewa na kijana mtanzania Isaya Yunge, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa spika janja ya Kaya inayoweza kufanya kazi kwa kumsikiliza binadamu. Isaya akihojiwa na Arnold Kayanda mjini New York Marekani anaanza kwa kueleza jinsi spika janja aliyoibuni yeye pamoja na wenzake inavyoanza kutekeleza ndoto hiyo ya Afrika kutafuta takwimu zao wenye.  Akisema “Smart Kaya kama akili bandia ya spika janja ina  uwezo wa kuvuna data na kuzitafsiri na kuweza kuziweka katika makundi ambayo serikali au watafiti wanaweza kuzitumia katika kufanya maamuzi. Kwa mfano tunaweza kutambua katika kaya za kiafrika kuna akina mama wangapi ni wajawazito. Kwa hivyo ukajua ni kiasi gani idadi ya watu inaongezeka na pia ukajua kiasi gani cha dawa upeleke hospital na ukaweza kujua watu hawa wako, mkoa gani, wilaya gani, tarafa gani au kijiji fulani.”

Kuhusu kwa nini anazishauri nchi za bara la Afrika kukusanya takwimu zake badala ya zile zinazotumia zaidi utaalamu wa nje, Isaya Yunge anaeleza,“ukiangalia matumizi ya mitandao ya kijamii barani Afrika, yanakua sana lakini hizo programu hazilipi ushuru katika bara la Afrika wala mabara hayafaidiki lakini pia hizo programu zinavuna data za Afrika na hivyo kuzitumia data hizo katika kuwatangazia watumiaji au wanunuzi wa vitu mbalimbali na hivyo  kuwalenga waafrika kuwafanyia matangazo ya biashara. Mimi nafikiri bara la Afrika waamke waweze kuona thamani ya data. Tunaamini kuwa tuna dhahabu, madini ya thamani  lakini kuna  dhahabu mpya ambayo ni dijitali, ambayo ni data, hii ni dhahabu kubwa sana. Bara la Afrika waamke waweze kushikilia data yao wao wenyewe.”