Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya wahamiaji na wakimbizi 22 kufa na TB libya ofisi ya haki za binadamu ina hofu kubwa

Watu walioshikiliwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakisubiri kuhamishiwa eneo salama. Pichani Msichana kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 19 akizungumza na mfanyakazi wa UNOCHA akisubiri kupanda basi kuelekea kituo cha mpito kabla ya kwenda Niger.
UN OCHA/GILES CLARKE
Watu walioshikiliwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakisubiri kuhamishiwa eneo salama. Pichani Msichana kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 19 akizungumza na mfanyakazi wa UNOCHA akisubiri kupanda basi kuelekea kituo cha mpito kabla ya kwenda Niger.

Baada ya wahamiaji na wakimbizi 22 kufa na TB libya ofisi ya haki za binadamu ina hofu kubwa

Wahamiaji na Wakimbizi

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR), leo imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya wakimbizi na wahamiaji wanaoshikiliwa katika kituo cha Zintan nchini Libya baada ya 22 kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na maradhi mengine .

Taarifa ya ofisi hiyo inasema tangu Septemba mwaka jana idadi ya vifo vya wakimbizi na wahamiaji katika kituo cha Zintan imeongezeka pia kukiwa na ripoti za watu kutoweka na usafirishaji haramu wa binadamu baada ya askari wa pwani wa Libya kuwakamata wale waliokuwa wakijaribu kwenda ng’ambo kupitia bahari ya Mediterania.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville amesema hadi sasa jumla ya watu 2,300 wameokolewa pwani ya Libya na kuwekwa kwenye vituo maalum.Na askari wa pwani wa Libya wameripoti kwamba tangu tarehe 30 Aprili wamepeleka mamia ya watu kwenye kituo cha Al-Khoms ambacho kipo chini ya usimamizi wa idara inayopambana na uhamiaji haramu, na idadi hii inajumuisha 203 waliopelekwa kituoni hapo Mei 23, hata hivyo kituo cha Al-Khoms kimeripoti kwamba kwa sasa kuna wahamiaji 30 tu waliopo. Ameongeza kuwa

SAUTI YA RUPERT COLVILLE

“Hususani hili linatutia hofu ukizingatia kwamba kuna ripoti za wahamiaji kuuzwa kwa ajili ya kushurutishwa kufanya kazi au kwa wasafirishaji haramu kuwaahidi watawasafirisha kwenda Ulaya. Pia kuna ripoti kwamba baadhi ya wanawake wanauzwa kwa ajili ya biashara ya ngono. Tumeorodhesha aina za unyanyasaji na ukatili ambazo wakimbizi na wahamiaji  wamekuwa wakiupitia Libya.”

Ofisi ya haki za binadamu imeitaka serikali ya Libya kuanzisha uchunguzi huru na wa kina mara moja ili kubaini wapi waliko watu hao ambao hawajulikani waliko.“Walinzi wa pwani wa Libya na idara ya kupambana na uhamiaji haramu ya nchi hilo ni lazima wahakikishe uwajibikaji kwa kila mtu anayeshikiliwa kituoni , na kuheshimu haki zao za binadamu. Tunaikumbusha serikali ya Libya kwamba kwakati mahabusu Anafi mikoni mwao kuna uwajibikaji wa serikali hapo, kwani Libya ina wajibu wa kulinda maisha ya watu wanaonyimwa uhuru ikiwemo kuwapa mahitaji ya lkazima ya huduma za afya.”

Hali katika kituo cha Zintan imeelezwa kuwa ni mbaya sana, si ya kibinadamu ni ya kudhalilisha au kuadhibu wanaoshikiliwa na pia inawea kuelezwa kuwa ni ya utesaji.

Jumla ya wahamiaji na wakimbizi 3400 bado wanashikiliwa mjini Tripoli kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, hivyo ofisi ya haki za binadamu “tunatoa wito kwa serikali ya Libya na Jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kwamba wahamiaji na wakimbizi wanaoshikiliwa katika vituo hivyo wanaachiliwa mara moja na kuangalia uwezekano wa kuwahamiasha, kwapeleka kwenye makazi mengine na kuwarejesha nyumbani kwa hiyari  haraka iwezekanavyo ikiwa pia ni opamoja na kusaka njia mbadala badala ya kuwaweka rumande vituoni.”