Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko ya ghafla yafurusha maelfu kusini-magharibi mwa Libya

Mji mkuu Libya, Tripoli
UNOCHA
Mji mkuu Libya, Tripoli

Mafuriko ya ghafla yafurusha maelfu kusini-magharibi mwa Libya

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya wakazi 2,500 wa mji wa Ghati, kusini-magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, wamelazimika kukimbia makazi yao kufuatia mafuriko ya ghafla yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha tarehe 28 mwezi uliopita wa Mei.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema kuwa kando ya kusababisha mafuriko na kufurusha maelfu, mvua hizo zimeshasababisha vifo vya watu wanne ilhali zaiid ya 30 wamejeruhiwa.

Msemaji wa UNHCR, mjini Geneva, Uswisi, Charles Yaxley amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa tayari watendaji wa shirika hilo wanaelekea eneo hilo ili kutoa usaidizi kwa sababu hivi sasa baadhi yao wanaishi na jamaa ilihali wengine wamesaka hifadhi kwenye maeneo ya shule na yale ya kijamii.

Bwana Yaxley amesema, “maji yameleta madhara makubwa pia kwenye  miundombinu kama vile barabara ambapo baraabra kadhaa zimejaa maji ilhali hospitali pekee mjini Ghat imefurika.”

Halikadhalika mtandao wa mawasiliano haufanyi kazi kwa siku kadhaa sasa na kwenye baadhi ya maeneo nyumba za makazi pamoja na mazao shambani vimeharibiwa kabisa na kwamba, “tegemeo la wengi kwenye mavuno siku za usoni liko mashakani.”

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa UNHCR, hivi sasa wakazi wengi wa Ghat wanategemea chakula cha msaada ambapo tayari shirika hilo limepeleka vifaa kama vile mahema, blanketi, maji ya kunywa, vifaa vya jikoni na nguo kwa ajili ya familia 400.

“Tunatarajia kuwa msaada huo utafika leo Ijumaa ambapo mdau wa UNHCR mjini Ghat, LibAid ameshaanza maandalizi ya kupokea na kusambaza vifaa hivyo haraka iwezekanavyo,” amesema Bwana Yaxley.

UNHCR inasema mvua zaidi zinatarajiwa kunyesha siku za usoni na hivyo changamoto zaidi zinataraijwa.