Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Sudan acheni kushambulia wahudumu wa afya

Waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum

Pande kinzani Sudan acheni kushambulia wahudumu wa afya

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema lina wasiwasi mkubwa juu ya athari za machafuko nchini Sudan kwa walio na mahitaji, wahudumu wa afya na vituo vya afya.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Mashairki ya Mediteranea Dkt. Ahmed Al-Mandhari amesema hayo katika taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo huko Cairo, Misiri.

“Uvamizi kwenye hospitali zilizoko mji mkuu wa Sudan, Khartoum umesababisha kufungwa kwa huduma za dharura, uhamishiaji wa wagonjwa usio na uhakika kwenda hospitali nyingine, kujeruhiwa kwa watendaji watano wa afya na wagonjwa pamoja na vitisho vingine,” amesema Dkt. Al-Mandari.

Amesema kuwa wahudumu wa afya wanaonekana kuwa walengwa kwa sababu tu wanatekeleza majukumu yao ya kutibu majeruhi na zaidi ya yote, “magari yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili ya kutibu waandamanaji majeruhi nayo yamatiwa moto na kuharibiwa, vifaa vya matibabu vimeporwa, wahudumu wa afya wameshambuliwa huku kukiwepo na ripoti za wahudumu wa afya wanawake kubakwa.”

Dkt. Al-Mandari amesema vitendo vya aina hiyo havikubaliki kabisa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na lazima vikomeshwe.

Amesema huduma ya afya hususan ya dharura inapaswa kulindwa dhidi ya muingilio wowote ule uwe wa kisiasa au kiusalama na kwamba wahudumu wa afya lazima waruhusiwe kufanya kazi yao ya kutibu majeruhi na wagonjwa bila ya kuwa na hofu ya usalama wao wenyewe.

Ametoa wito kwa pande zote kusitisha chuki na kupatia kipaumbele usalama wa watoa huduma za afya na wagonjwa.

Dkt. Al-Mandari amesema WHO kwa upande wake huku ikishirikiana na Wizara ya Afya nchini Sudan wanaendelea kuhakikisha kuwa hospitali zinaendelea kufanya kazi na huduma muhimu zinafikishwa nchini humo.

Tayari malori manane yenye vifaa vya matibabu vya WHO yamewasili mjini Khartoum na maeneo mengine muhimu ili kuimarisha huduma kwenye vituo vya afya.