Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya kipindupindu Sudan kuanza katikati ya mwezi huu- WHO

Katika jimbo la Blue Nile nchini Sudan, mtoto akinawa mikono kwenye kijiji ambako UNICEF imekuwa ikiendesha kampeni za usafi na kujisafi ili kuepukana na ugonjwa wa Kipindupindu.
© UNICEF
Katika jimbo la Blue Nile nchini Sudan, mtoto akinawa mikono kwenye kijiji ambako UNICEF imekuwa ikiendesha kampeni za usafi na kujisafi ili kuepukana na ugonjwa wa Kipindupindu.

Chanjo dhidi ya kipindupindu Sudan kuanza katikati ya mwezi huu- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema awamu ya kwanza ya utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa Kipindupindu kwenye majimbo mawili ya Blue Nile na Sinnar nchini Sudan itaanza katikati ya mwezi huu wa Oktoba.

Tangazo hilo la WHO linafuatia thibitisho la mlipuko wa Kipindupindu kwenye jimbo la Blue Nile nchini humo tarehe 8 mwezi uliopita wa Septemba.

Msemaji wa WHO mjini Geneva, Uswisi, Tarik Jasarevic amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa hadi jumamosi iliyopita wagonjwa 215 walikuwa wamethibitishwa na kati yao wanane wamefariki dunia.

Hivi sasa shirika hilo kwa ushirikiano na Wizara ya afya ya Sudan na wadau wa kitaifa na kimataifa wanajiandaa kuchukua hatua ya kinga dhidi ya Kipindupindu  kwenye majimbo hayo mawili na mengine 6 yenye uwezekano wa kukumbwa na mlipuko huo ambayo ni White Nile, Kassala, Gedaref, Gezira, Khartoum na Mto Nile.

Tayari WHO imeanzisha vituo vitatu vya tiba dhidi ya kipindupindu kwenye jimbo la Blue Nile na vituo 6 vya karantini ya wagonjwa hao jimboni Sinnar.

Halikadhalika wataalamu wa kusaidia harakati za kinga dhidi ya Ebola wamepelekwa jimbo ni Blue Nile huku WHO ikisema inafuatia kwa karibu kiwango cha  ubora wa maji katika jamii sambamba na kuzuia maambukizi zaidi kwenye vituo vya tiba.

Kuhusu chanjo hiyo kwenye majimbo  ya Blue Nile na Sinnar, Bwana msemaji wa WHO mjini Geneva, Uswisi, Tarik Jasarevic amesema,

(Sauti ya Tarik Jasarevic)

Kufuatia ombi la wizara ya afya ya Sudan na wadau wa kimataifa,  WHO itaunga mkono na UNICEF kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu inayofadhiliwa na fuko la chanjo duniani, GAVI ikilenga watu milioni 1.6 kwenye wilaya 8 za majimbo hayo mawili yaliyothibitishwa kuwa na kipindupindu. Chanjo ya kipindupindu ni kwa kila mtu aliye na umri wa zaidi ya mwaka mmoja, wakiwemo wanawake wanaonyonyesha ma wajawazito. Kama mjuavyo chanjo ya kipindupindu ni dozi mbili kwa hiyo awamu ya kwanza itaanza katikati ya Oktoba.”

WHO inakadiria kuwa itahijitaij kati ya dola milioni 10 hadi 15 ili kudhibiti  mlipuko wa sasa kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita ili kuweza kufikia majimbo hayo 8 yaliyo hatarini.

Fedha hizo zitatumika kushughulikia  masuala ya afya, maji safi na salama, chakula salama, mazingira safi, lishe bora na huduma bora za afya zipatikane na zitolewe na wataalamu wenye ujuzi.

Mlipuko wa kipindupindu wa kuanzia Agosti 2016 hadi Machi 2018 nchini Sudan ulikumba wagonjwa 36,962 katika majimbo 18 ya Sudan na kusababisha vifo vya watu 823 ambao kati yao asilimia 15 walikuwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Tathmini ya mlipuko huo ndio imetumika kupanga mikakati ya kudhibiti mlipuko wa sasa.