Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya CAR yasihi kiongozi wa 3R akabidhi mbele ya sheria wauaji wa Paoua

Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Yaye Nabo Sène/OCHA
Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Serikali ya CAR yasihi kiongozi wa 3R akabidhi mbele ya sheria wauaji wa Paoua

Amani na Usalama

Kufuatia mauaji ya watu zaidi ya 30 yaliyofanywa na kikundi kilichojihami cha 3R kwenye jimbo la Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, serikali nchini humo imemtaka kiongozi wa kikundi hicho ahakikishe wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ujumbe wa serikali ukiambatana na wawakilishi wa jumuiya ya kiuchumi ya  nchi za Afrika ya Kati, ECCAS, na wawakilishi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA wakianza safari kuelekea Niem-Yelewa, mji ulio kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo ambako ni ngome ya kikundi cha 3R.

Lengo la ziara hii kwenye jimbo la Bour ni kufahamu hasa sababu za mauaji hayo na kuwasilisha ombi maalum kwa kiongozi wa kikundi hicho cha 3R, Bi Sidi Souleymane ajulikanaye pia kama Sidiki kuwafikisha wahusika wote wa mauaji hayo mbele ya sheria,  ingawa tayari ameshakabidhi watuhumiwa watatu.

Hatua hii  ya kuwasilisha ombi hilo kwake linazingatia kuwa kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano mapya ya amani mwezi Februari mwaka huu kati ya serikali na vikundi 14 vilivyojihami, Sidiki alichaguliwa kuwa mshauri maalum wa kijeshi kwa Waziri Mkuu, akihusika na ujumuishaji kwenye jeshi la serikali wanajeshi kutoka vikundi mbalimbali vilivyojihami.

Henri Wanzet-Linguissara ni Waziri wa Mambo ya Ndani, CAR anasema kuwa "sidiki yuko tayari kutoa ushirikiano na mkondo wa sheria. Anakubali kuwa watuhumiwa wanatoka kikundi chake cha 3R lakini walitenda kosa bila maelekezo yake. Yuko tayari kuwakabidhi mbele  ya sheria.”

Hata  hivyo akiwa na hofu ya kusaliti kundi lake, Sidiki anasema waliofanya mauaji ni wahalifu tu na kwamba, "tunaf uraha kwamba wamefika hapa tuzungumze kuhusu mauaji huko Koundjili, Lemouna, na Bohong. HAtuwafahamu watekelezaji ambao wameenda kuua raia wasio na hatia. Hatuwezi kuruhusu wahalifu waishi na sisi. Tutawafikisha mbele ya sheria ili wajibu matendo yao.”

Mauaji huyo Paoua ni kitendo cha kwanza cha kikatili kufanyika tangu mkataba utiwe saini mwezi Februari ambapo Naibu Mkuu wa MINUSCA Kenneth Gluck anasema,  “tupo hapa kuhakikisha kuwa kikundi cha 3R kinasalia mdau katika amani na kinaahidi kukabidhi wahusika wote wa mauaji kwa mamlaka ya CAR ili wafikishwe mahakamani.”

MINUSCA inatarajia kuwa 3R itachukua hatua za haraka kusalimisha silaha kwa mujibu wa mpango wa kitaifa wa kusalimisha silaha ulioanzishwa kwa mujibu wa mkataba wa amani.