UNHCR yasaidia kuhamisha mahabusu 96 kutoka Somalia, Eritrea na Ethiopia

4 Juni 2019

Watu 96 wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha Zintan mjini Tripoli Libya sasa wamehamishiwa kwenye eneo salama ambapo wanakusanywa na kusafirishwa kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa UNHCR watu hao ni kutoka Somalia, Eritrea na Ethiopia wakiwemo Watoto wachanga wawili. Shirika hilo linawapatia msaada wa chakula , malazi, huduma za afya zikiwemo za kisaikolojia , mavazi, viatu, vifaa vya kujisafi na mablanketi na watasalia katika kituo hicho cha mapokezi wakisubiri kusafirishwa nje ya nchi. Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa UNHCR Barbar Baloch amesema watu hao walikuwa wakishikiliwa katika mazingira magumu na yasiyostahili

 

(SAUTI YA BARBAR BALOCH)

“Hali katika kituo cha Zintan nim baya, makazi yamefurika na hakuna hewa ya kutosha, katika baadhi ya sehemu za kituo hicho vyoo vimejaa na kufurika na sasa vinahitaji ukarabati haraka, matokeo yake taka ngumu na uchafu mwingine vimerundikana ndani ya kituo hicho kwa siku kadhaa na kuwa ni tishio kubwa kwa afya.”

Ameongeza kuwa pia mvutano baina ya mahabusu unaongezeka kwa sababu wametaharuki na kukosa msaada.

Jumla ya wakimbizi na wahamiaji 654  wanashikiliwa katika kituo cha Zintan na UNHCR inasisitiza kwamba hatua zote muhimu zichukuliwe ili kuhakikisha mahabusu wote waliosalia wanahamishwa kituoni hapo. Libya hivi sasa kwa mujibu wa UNHCR ina matatizo mengi ikiwemo vita vinavyoendelea jambo linalofanya kuwa vigumu kuhifadhi wakimbizi na wahamiaji.

Wengi wa watu hao wanaoshikiliwa ni wale waliookolewa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterranea. Hadi kufikia Mei mwaka huu takribani watu 1224 wamerejeshwa Libya na askari wa ulinzi wa ufukweni.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud