Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 3,000 wamekufa au kupotea wakijaribu kuvuka bahari kwenda Ulaya:UNHCR 

Wahamiaji kutoka Ethiopia wakiwa kwenye pwani ya Obock, Djibout
© IOM 2020/Alexander Bee
Wahamiaji kutoka Ethiopia wakiwa kwenye pwani ya Obock, Djibout

Zaidi ya watu 3,000 wamekufa au kupotea wakijaribu kuvuka bahari kwenda Ulaya:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu 3,000 walikufa au kutoweka walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania na Atlantiki mwaka jana kuelekea barani Ulaya.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, inatoa wito wa msaada na hatua za haraka ili kuzuia vifo zaidi na kuwalinda wakimbizi na waomba hifadhi wanaoanza safari hizi hatari za nchi kavu na baharini. 

Kwa mujibu wa shirika hilo mwaka jana 2021, watu 1,924 waliripotiwa kufariki dunia au kupotea wakiwa safarini kupitia bahari ya Mediterania, huku wengine 1,153 wakipoteza maisha au kupotea kwenye njia ya kupitia baharini ya Kaskazini Magharibi mwa Afrika kuelekea visiwa vya Canary.  

Idadi ya vifo vilivyoripotiwa mwaka 2020 ilikuwa 1,544 kwa njia hizo mbili. UNHCR inasema inatia hofu kwamba, tangu mwanzo wa mwaka huu, watu wengine 478 pia wamekufa au kupotea baharini. 

Ajali nyingi ni za boti zilizojaa pomoni 

Shirika hilo la wakimbizi limesema safari nyingi za vivuko vya baharini zilifanyika katika boti zilizojaa pomoni, zisizostahili kwa safari hizo za majini, na zenye kujazwa hewa na nyingi kati ya hizo zilipinduka au kuharibika na kusababisha kupoteza Maisha ya watu wengi.  

Safari za baharini kutoka mataifa ya pwani ya Afrika Magharibi kama vile Senegal na Mauritania hadi visiwa vya Canary ni ndefu na za hatari na zinaweza kuchukua hadi siku 10 kuwasili limesema shirika hilo la wakimbizi.  

Limeongeza kuwa boti nyingi zilizama au kupotea bila kujulikana zilipo  katika maji hayo. 

UNHCR inasema njia za nchi kavu pia zinaendelea kuwa hatari sana, ambapo huenda idadi kubwa zaidi ya watu walikufa katika safari kupitia Jangwa la Sahara na maeneo ya mpakani ya mbali, katika vituo vya kizuizini, au walipokuwa katika utumwa wa wasafirishaji haramu.  

Miongoni mwa orodha ya dhuluma zinazoripotiwa na watu wanaosafiri katika njia hizi ni pamoja na mauaji ya kiholela, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria na kiholela, unyanyasaji wa kingono na kijinsia, kazi za kushurutishwa, utumwa, ndoa za kulazimishwa na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu. 

Boti ikisafirisha wahamiaji katika pwani ya Libya.
© SOS Mediterranee/ Anthony Jean
Boti ikisafirisha wahamiaji katika pwani ya Libya.

COVID-19 imeathiri safari hizo 

Kwa mujibu wa UNHCR janga la COVID-19 na kufungwa kwa mipaka husika kulikoendelea mwaka 2021 pia kumeathiri harakati za kuelekea Afrika Kaskazini na nchi za pwani za Ulaya, na wakimbizi na wahamiaji wengi waliokata tamaa wakigeukia wafanyabiashara wa magendo ili kuwezesha safari hizi hatari. 

UNHCR inaonya kwamba kuendelea kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na migogoro, kuzorota kwa hali ya kijamii na kiuchumi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi kunaweza kuongeza hali ya watu kuhama na kusonga mbele hatari. 

Ikizindua mkakati mpya uliorekebishwa wa ulinzi na suluhu kwa wakimbizi wanaosafiri katika safari hatari kwenye njia za kuelekea Ulaya kupitia bahari ya Mediterania na Atlantiki, UNHCR inataka dola za Marekani milioni 163.5 kusaidia na kulinda maelfu ya wakimbizi na watu wengine. 

UNHCR inaomba usaidizi ili kusaidia kutoa njia mbadala za maana kwa safari hizi hatari na kuzuia watu kuwa wahanga wa wasafirishaji haramu.  

Mtazamo huo unatoa wito wa kuongezeka kwa usaidizi wa kibinadamu, usaidizi na suluhu kwa watu wanaohitaji ulinzi wa kimataifa na manusura wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. 

Ombi litasaidia nchi 25 

UNHCR inasema ombi hilo litasaidia nchi 25 katika maeneo manne tofauti yaliyounganishwa na njia zile zile za ardhini na baharini ambazo hutumiwa na wahamiaji, wasaka hifadhi na wakimbizi.  

Na ni pamoja na nchi za asili, kuondoka, hifadhi ya kwanza, usafiri na nchi wanakoenda. 

Wakati huo huo, UNHCR inazitaka nchi kujitolea kuimarisha hatua za kibinadamu, maendeleo na amani ili kushughulikia ulinzi na kutatua changamoto za watu wao. 

UNHCR pia inatoa wito kwa mataifa katika kanda barani Afrika na Ulaya  kuimarisha mifumo ya kisheria na uwezo wa kufanya kazi katika mipaka ya nchi kavu na baharini na katikati mwa miji, na kuhakikisha kuna njia mbadala za kuaminika za safari hatari kwa kujumuisha, na kuimarisha programu za vijana na maendeleo ya kijamii. 

Shirika hilo limeongeza kuwa mataifa lazima yahakikishe ufikiaji usiona vikwazo wa misaada ya kibinadamu hasa utoaji wa huduma muhimu kwa watu wanaohama au waliokwama njiani, wanaozuiliwa baharini, au waliowekwa kizuizini, na kubaini kama wana mahitaji ya ulinzi wa kimataifa. 

“Wakishindwa kufanya hivyo, wakimbizi, waomba hifadhi, wakimbizi wa ndani na wengine wataendelea kusonga mbele katika safari za hatari kutafuta usalama na ulinzi. Watu wengine, wakiwemo wahamiaji, wataendelea kusaka maisha bora, wakitumaini kupata kazi au fursa za elimu mahali pengine kwa kukosekana kwa njia za kisheria za dharura au za muda mrefu za uhamiaji salama na wa utaratibu.” limesisitiza shirika hilo.