Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu sita walifariki dunia kila siku wakivuka Mediteranea kuelekea Ulaya 2018

Mwanamke akilia baada ya kuokolewa baharini nchini Libya
UNHCR/Hereward Holland
Mwanamke akilia baada ya kuokolewa baharini nchini Libya

Watu sita walifariki dunia kila siku wakivuka Mediteranea kuelekea Ulaya 2018

Amani na Usalama

Watu sita walifariki kila siku mwaka jana wakiwa safarini kuvuka bahari ya Mediterenea kuingia bara Ulaya, safari hiyo ikitajwa kama ni ya hatari zaidi kupitia bahari kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNHCR iliyotolewa leo, takriban watu 2,275 wamezama au kutowekea bahari ya Mediteranea mwaka 2018. Licha ya kwamba bara Ulaya ilishuhudia idadi ndogo sana ya wakimbizi na wahamiaji kwa kipindi cha miaka mitano ikielezwa watu 139,300 waliwasili  ambapo 65,400 wakiwasili Uhispania, 50,500 Ugiriki na 23,400 Italia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filipo Grandi amesema, “kuokoa maisha sio suala la kuchagua, au siasa lakini ni wajibu wa miaka mingi’. Na kwamba, “tunaweza kukomesha ajali hizo kwa kuwa na ujasiri na maono ya kuona mbali zaidi ya boti nyingine ijayo na kuazimia ushirikiano wa muda mrefu ambao unayhamini maisha ya mtu na hadhi yake kama nyenzo.”

Watu wenye kiwewe wanawekwa baharini kwa muda mrefu

Mwaka jana, mabadiliko ya sera kwenye mataifa ya Ulaya yamesababisha matukio mengi ambapo watu wameachwa baharini kwa siku nyingi kwa sababu boti zinazowabeba zimenyimwa ruhusa kutia nanga.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, boti za kuokoa watu na wafanyakazi wake walikabiliwa na vikwazo katika operesheni zao. Aidha katika safari za Libya kuelekea Ulaya, mtu mmoja kati ya 14 waliowasili Ulaya alifariki dunia baharini. Hii ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na idadi ya waliofariki mwaka 2017 ambao walikuwa ni  mtu mmoja kwa kila watu 38 waliowasili.

UNHCR imeangazia maamuzi ya walinzi wa pwani ya Libya kuimarisha operesheni zao 2018 ambapo watu zaidi ya wanane kwa kila watu kumi waliookolewa baharini walirejeshwa Libya ambako walikabiliwa na hali mbaya wakiwa vizuizini ikiwemo, ukosefu wa chakula, magonjwa na vifo kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR.

Wakikabiliwa na hatari hiyo nchini Libya ambako kunashuhudiwa mzozo na msukosuko wa kisiasa tangu kuondolewa kwa rais Muammar Gadaffi mwaka 2011, UNHCR inakadiria kwamba idadi kubwa ya boti zinazowasafirisha wakimbizi na wahamiaji zitalenga kuepuka walinzi wa pwani ya Libya na kuelekea Malta na Italia mwaka huu.

Kufika Ulaya ndio hatma katika safari hii iliyo kama jinamizi

Idadi kubwa ya watu wanaowasili Uhispania ni kutoka Morocco na Guinea ikiwa ni watu13,00o kwa kila nchi huku wengi wanaowasili Italia wanatokea Tunisia, ambao ni watu 5,200 na Eritrea 3,300

Watu wengi kutoka Afghanistan walielekea Ugiriki  jumla ya  9,000 wakifuatiwa na wakimbizi kutoka Syria waliokuwa 7,900.

Kuwasili ulaya ilikuwa ni awamu ya mwisho ya safari hii ya jinamizi ambako wahamiaji walikabiliwa na unyanyasaji, kubakwa, ukatili wa kingono na tishio la kutekwa nyara na kushikiliwa hadi kulipiwa fidia. UNHCR katika ripoti yake inatoa wito kwa mataifa kusambaratisha mitandao ya wasafirishaji haramu na kuwashtaki wanaotekeleza vitendo hivyo pamoja na kuwawajibisha kisheria.

Licha ya mkwamo wa kisiasa miongoni mwa mataifa ya bara Ulaya yameombwa kubuni njia ya kukabiliana na uokozi bahari kama ilivyopendekeza UNHCR na shirika la uhamiaji  IOM mwezi Juni mwaka jana, ripoti imekaribisha hatu ya matifa hayo kuelezea utayari wake wa kuwapa hifadhi watu waliokoolewa Mediteranea , na huenda ni “msingi muhimu kwa suluhu ya kudumu.” Aidha mataifa yametoa maelfu ya fursa za uhifadhi kwa wakimbizi wanaohamishwa kutoka Libya.