Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Gaza yapamba moto, Guterres asihi pande husika zijizuie

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres
UNFCCC Secretariat/James Dowson
Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres

Mapigano Gaza yapamba moto, Guterres asihi pande husika zijizuie

Amani na Usalama

Ghasia zikiendelea kushika kasi huko ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati, kati ya wanamgambo wa kipalestina na Israel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anafuatilia hali ilivyo huku akiwa na wasiwasi mkubwa.

Vyombo vya habari vinaripoti kwamba wanamgambo wa kipalestina wamerusha makombora 600 ya roketi mwishoni mwa wiki kuelekea upande wa Israel ambapo jeshi la Israel liliingia kati na kwamba waisrael watatu waliuawa ilhali upande wa Gaza watu 15 wameripotiwa kuuawa.

Taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York, Marekani, imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa kinachoendelea kinazidi kuhatarisha hali iliyopo na pia kusababisha vifo vya watu wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Amelaani vikali urushaji wa makombora kutoka Gaza kuelekea Israel hususan ulengaji wa maeneo ya raia.

Katibu Mkuu amesihi pande zote kujiuzui na kuacha mara moja mashambulizi na badala yake zirejelee maelewano yaliyokuwepo miezi michache iliyopita.

Msemaji huyo wa Katibu Mkuu amesema, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa Nickolay Mladenov anashirikiana kwa karibu na Misri pamoja na pande husika ili kurejesha utulivu.

Hapo jana Bwana Mladenov alitoa taarifa yake akitaka pande husika zirejeshe utulivu.