Ghasia Gaza zinatowesha maelewano yaliyopatikana- Mladenov

4 Mei 2019

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mchakato wa amani Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov ameelezea masikitiko yake juu ya mwendelezo wa ghasia na kupoteza maisha ya watu huko Ukanda wa Gaza.

Vyombo vya habari vimenukuu jeshi la Israel likisema kuwa makombora yapatayo 200 yalirushwa na wapiganaji huko Gaza leo Jumamosi kuelekea upande wa Israel ambapo jeshi hilo lilijibu mashambulizi. Wapalestina watatu waliuawa akiwemo mama mmoja na binti yake.

Katika taarifa yake aliyotoa leo huko mjini Yerusalem, Bwana Mladenov ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa wa mashambulizi ya leo huko Gaza na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Amesema “Umoja wa Mataifa unashirikiana na Misri na pande zote husika ili kurejesha utulivu na natoa wito kwa kukoma kwa mwendelezo wa mapigano. Tafadhali turejelee maelewano yaliyokuwepo miezi michache iliyopita, yeyote ambaye anasaka kuondoa maelewano hayo atawajibika.”

Bwana Mladenov amesema kuendelea na ghasia kutapoteza mafaniko yote yaliyopatikana na kwamba mzunguko wa ghasi lazima ukome.

“Mwenendo wa sasa unapoteza maendeleo  yaliyopatikana wiki zilizopita za kuondoa machungu ya wakazi wa Gaza, ya kuondoa vikwazo na kusaidia maridhiano ya kipalestina,” amesema mratibu huyo maalum.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud