Kuwanyima chakula wahamiaji rumande Hungary inatia hofu:Bachelet

3 Mei 2019

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema ametiwa hofu na ripoti kwamba wahamiaji wanaoshikiliwa rumande katika vituo mbalimbali nchini Hungary wamekuwa wakinyimwa chakula kwa maksudi kitendo ambacho ni kinyume na wiwango na sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa sharia za Hungary wahamiaji na waomba hifadhi wasio na haki ya kuishi nchini humo wanakamatwa mara moja na kuwekwa rumande kwenye vituo vya muda wakati wakisubiri mchakato wa kuomba hifadhi au hadi pale watakaporejeshwa walikotoka.

Kwa mujibu wa Bachelet katika vituo hivyo wanakabiliwa na mchakato wa kuomba hifadhi na kurejeshwa kwa lazima ambao umeshindwa kutathimini vyema hali ya kila mmoja.”Tunatiwa hofu  kutokana na kutokuwepo kwa mchakato unaotathimini hali ya kila mmoja ambao unahitajika ili kuhakikisha kunyimwa uhuru chaguo la nadra na kwamba hatari zote zitakazomzuia mtu kurejea atokako zinazingatiwa.”

Licha ya ukweli huo Bachelet amesema ofisi ya Hungary ya masuala ya uhamiaji na kuomba hifadhi yanaanza mchakato kwa mtazamo wa kufukuza watu ambao maombi yao yamekataliwa nchini humo, na wahamiaji hawapatiwi tena chakula. Wakisubiri kufukuzwa watu wazima ukiacha kina mama wajawazito na wanaonyonyesha , wengine wananyimwa chakula makusudi hali ambayo inaweza kuwasabibishia utapiamlo n ani hatari kwa afya zao na nikinyume na ubinadamu.

Kwa mujibu wa duru za habari tangu mwezi Agosti 2018 takriban wahamiaji 21 wanaosubiri kurejeshwa kwa nguvu walikotoka wamekuwa wakinyimwa chakula na mamlaka ya Hungary wengine hadi siku tano.

Amesema ingawa anatambua serikali ya Hungary imeahidi kukomesha hatua hiyo lakini ofisi ya haki za binadamu inasikitika kwamba ripoti zinaonyesha vitendo hivyo vinaendelea.

Ofisi hiyo imezikumbusha nchi kuhusu wajibu wake chini ya sharia za kimataifa kuhusu kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na pia kutambua kwamba ni kuyaweka rehami maisha ya watu hao wanapowalazimisha kujerea walikotoka ambako wengi huwa katika hatari ya kifo, mateso, unyanyasajina ukatili. Na kwamba kufanya hivyo ni kukikua sharia za kimataifa n ani ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter