Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR leo limeitaka serikali ya Ugiriki kushughulikia tatizo la msongamano kwenye kituo cha mapokezi cha baharini Aegean na vituo vya utambuzi wa wahamiaji na waomba hifadhi (RICs) ambavyo hujulikana kama vituo mashuhuri.
Kwa mujibu wa shirika hilo vituo hivyo vimefurika pomoni na hii inamaanisha kwamba maelfu ya waomba hifadhi na wahamiaji wakiwemo watoto wengi, wanaishi katika mazingira duni na hali mbaya inayoendelea kuzorota kila uchao.
Baadhi ya watu hao wamekuwa wakiishi katika vituo hivyo kwa zaidi ya miezi sita. Hivi sasa UNHCR inatoa wito kwa mamlaka ya Ugiriki kuchapuza mchakato wa kuwahamisha kwenda nchi kavu wanaokidhi vigezo, kupanua wigo wa vituo hivyo vya mapokezi, na kutoa malazi mbadala kwa watu wasiojiweza na walioko hatarini.
UNHCR imeongeza kuwa hali hivi sasa imefikia pabaya katika kituo cha Moria kwenye kisiwa cha Lesvos ambako zaidi ya waomba hifadhi na wahamiaji 7,000 wanabanana kwenye malazi yaliyojengwa kumudu watu wasiozidi 2,000 huku ikielezwa kuwa robo ya watu hao ni watoto.