Hungary tupilieni mbali mswada wa sheria zitakayowaathiri wakimbizi: UNHCR

Wahamiaji kutoka Pakistani huko Kos, Ugiriki waonyesha ramani waliyopokea kuhusu kufungwa kwa mpaka wa Hungary na ikipendekeza kupitia Croatia. Picha: IOM

Hungary tupilieni mbali mswada wa sheria zitakayowaathiri wakimbizi: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limetoa wito kwa serikali ya Hungary kuachana na mswada wa sheria zinazotarajia kuwasilishwa bungeni ambazo zitabana uwezo wa mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s na watu binafsi kuwasaidia waomba hifadhi na wakimbizi.

Shirika hilo linasema lina wasiwasi mkubwa na mapendekezo hayo, endapo yatapitishwa yatawanyima msaada na huduma muhimu watu ambao wamelazimika kukimbia makwao na pia kuongeza mvutano miongoni mwa jamii na tabia ya chuki dhidi ya wageni.

Akisisitiza kuhusu hilo Pascale Moreau mkurugenzi wa UNHCR barani Ulaya amesema kuomba hifadhi ni haki ya msingi ya binadamu na inatia hofu kuona serikali inalenga jukumu la kibinadamu la kuwasaidia watu wanaoomba hifadhi, hivyo kuongeza sheria za kuwabana watu au mashirika yanayowasaidia waomba hifadhi na wakimbizi kutasababisha watu hao kuwa katika hali ngumu na kuwanyima huduma muhimu kama za afya, msaada wa kisaikolojia, nyumba, elimu, ajira, fursa ya kupata taarifa na msaada wa kisheria. Hali ambayo pia itaathiri jamii zinazowahifadhi.

Hivyo amesisitiza serikali ya Hungary kusitisha hatua zozote ambazo zitaongeza madhila kwa watu hao ambao wanasaka usalama.

Serikali ya Hungary leo imetangaza nia yake ya kuongeza vikwazo katika fungu la sheria ambazo awali ziliwasilishwa bungeni mwezi Februari mwaka huu. Bwana Moreau amesema tangu Januari Hungary imefunga mipaka yake na imefanya kuwa vigumu sana watu kuwasilisha maombi ya hifadhi au ukimbizi Mwaka mzima uliopita ni watu 1200 pekee ndio waliopewa hifadhi nchini humo.

TAGS: UNHCR, Hungary, wakimbizi, waomba hifadhi, NGO’s