Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafaniko ya UNISFA yalindwe katika kutatua suala la Abyei-Lacroix

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa ulinzi wa muda kwenye jimbo la Abyei (UNISFA)  ukipiga doria Abyei
IRIN/Hannah McNeish
Mpango wa Umoja wa Mataifa wa ulinzi wa muda kwenye jimbo la Abyei (UNISFA) ukipiga doria Abyei

Mafaniko ya UNISFA yalindwe katika kutatua suala la Abyei-Lacroix

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumanne limekutana jijini New York, Marekani kujadili hali ya Sudan na Sudan Kusini hususan eneo gombaniwa la Abyei.

 

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix ameliambia baraza hilo kwamba ni muhimu kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana na Umoja wa Mataifa katika eneo la Abyei mpakani mwa Sudan na Sudan Kusini (UNISFA) pamoja na jamii Abyei yalindwe na yatumike kusongesha maazimio ya kisiasa katika kutatua maswala ya mpakani kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Bwana Lacroix amesema licha ya matukio ya hapa na pale ya vurugu, hali eneo la Abyei inasalia kuwa tulivu akiongeza kwamba operesheni za ujumbe wa muda wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Abyei, UNISFA zinaendeleza shughuli zake.

Amesema “UNISFA inaendelea kutekeleza nafasi ya kulinda usalma katika eneo la Abyei na mipakani, hatahivyo, ujumbe huo unaweza tu kuhakikisha mazingira salama kwa pande husika, ambazo mchango wao ni muhimu katika kuhakikisha hatua zinapigwa kuelekea amani.”

Mkuu huyo ameongeza kwamba, “ninatiwa moyo na kuimarika kwa mahusiano baina ya nchi mbili hizo katika kipindi cha mwaka mmoja kama ilivyodhihirishwa na nafasi ya Sudan katika kunga mkono makubaliano ya amani yaliyofikiwa n apande husika za Sudan Kusini na kurejea kuendesha kwa pamoja  operesheni za mafuta.”

Bwana Lacroix amesisitiza kwamba, “Sudan na Sudan Kusini zinapaswa kuendelea hivyo hivyo na kutanua ushirikiano ili kusongesha mbele makubaliano ya kusitisha mizozo yao.”

Kwa upande wake mwakilishi maalum wa katibu Mkuu kwa ajili ya pembe ya Afrika Parfait Onanga-Anyanga amesema kwamba kuondolewa madarakani kwa rais wa Sudan, Omar al-Bashir kunatia wasiwasi kuhusu pengo la mmoja wa watekelezaji wa mkataba wa amani wa Sudan Kusini kuathiri utekelezaji wake. Aidha kuna wasiwasi kuwa juhudi za amani katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile huenda zikaathirika.

Kwa mantiki hiyo bwana Onanga-Anyanga amesema, “kwa kuzingatia hali ya sasa, nchi mbili hizo zinapaswa kutiwa moyo kuzingatia utekelezaji wa makubaliano hayo. Sudan inapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano mapya ya amani na Sudan Kusini inahitaji kuchukua nafasi katika kutatua mzozo ulioko Sudan.”

Ameongeza kuwa, “mabadiliko ya kisiasa nchini Sudan huenda yakatoa fursa kwa ajili ya kuelezea mahusiano na wenyeji katikati na vitongojini kwa njia ambayo inatokomeza ubaguzi kwa misingi ya kabila, dini, na eneo atokako mtu.”

Akihutubia baraza hilo mwakilishi wa kudumu wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa balozi, Omer Ahmed Mohamed Ahmed amesema, “ni wazi kuwa utaratibu wa Abyei ambao ni sehemu ya makubaliano ya amani ya kina (CPA) ya 2007, ni nguzo muhimu ya kazi za baraza hilo na utaratibu unasema bila swali kwamba Abyei ni sehemu muhimu ya mamlaka ya Sudan. Hili linajulikana katika historia kwa hiyo makubaliano yoyote yatokanayo na CPA yanapaswa kuzingatia hilo.”

Kwa upande wake, mwakilishi wa kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja huo bi. Cecilia A.M. Adeng amesema kwamba serikali yake, “inashukuru hatua za UNISFA na mamlaka ya mataifa hayo mawili imepiga hatua na juhudi za kufanikisha amani ya kudumu katika mataifa hayo mawili.

Ameongeza kuwa, “tuna matumaini kwamba hatua iliyoanzishwa na mataifa haya mawili yenye udugu katika kutatua suala la Abyei itaendelea kwa ajili ya kutengeneza mazingira mazuri kufikia muafaka wa hali ya Abyei.”