Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuweke kanuni za biashara ya vyakula visivyosindikwa ili kudhibiti idadi  ya tipwatipwa duniani- FAO

Chakula chenye virutubisho vya kutosha vya lishe kinaweza kumwondoa mtu hususani watoto katika hatari ya kupata magonjwa.
World Bank/Maria Fleischmann
Chakula chenye virutubisho vya kutosha vya lishe kinaweza kumwondoa mtu hususani watoto katika hatari ya kupata magonjwa.

Tuweke kanuni za biashara ya vyakula visivyosindikwa ili kudhibiti idadi  ya tipwatipwa duniani- FAO

Afya

Jukwaa la kimataifa kuhusu usalama wa chakula na biashara likikunja jamvi hii leo huko Geneva, Uswisi, mashirika  ya Umoja wa Mataifa yametaka mataifa kuzingatia siyo tu usalama wa chakula kinacholiwa bali pia mchango wake katika afya ya mlaji ili kudhibiti ongezeko la matipwatipwa duniani.

Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva akizungumza kwenye mkutano huo amesema nchi nyingi duniani zinategemea zaidi vyakula vya kuagizwa kutoka nchi zao ili kukidhi mahitaji ya chakula kwa wananchi wao.

“Bahati mbaya vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi ndio vinavyofanya vyema kwenye biashara ya kimataifa kwa urahisi wake wa kusafirishwa na kuhifadhiwa kuliko vyakula ambavyo havijasindikwa,” amesema Bwana da Silva.

Amesema biashara ya bidhaa kama hizo imesababisha ongezeko kubwa la watu wenye uzito wa kupindukia hususan kwenye nchi zinazotegemea vyakula vya kuagizi kutoka nje ya nchi zao hususan nchi za visiwa vya Pasifiki na Karibea.

“Natoa wito kwa jamii ya kimataifa kusongesha na kuanzisha kanuni za biashara ambazo zitachochea ulaji wa vyakula vyenye lishe bora,” amesema Mkuu huyo wa FAO.

Akizungumza kwenye jukwaa hilo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, “chakula kinavuka mipaka ya kitaifa. Chakula kilichozalishwa kwenye nchi moja kinawwza kufika upande mwingine wa duniani ndani ya saa 24 na kusambazwa kwenye migahawa, maduka na majumbani. Hii ina maana kwamba hakuna suala la usalama wa chakula kwa matajiri au maskini kwa hiyo afya ya kila mtu bila kujali popote alipo na nini anakula inapaswa kulindwa kwa usawa bila ubaguzi.”

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la biashara duniani, WTO Roberto Azevêdo akichangia mada hiyo amesema,  "suala la mtu kupata chakula kilicho salama ni muhimu ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Kwa hiyo ni vyema kujadili ni kwa vipi sera kuhusu chakula, afya na biashara vinaweza kuoanishwa na kufanikisha malengo hayo.”

Bwana Azevedo amesema ni lazima kutumia fursa ya teknolojia ambazo zinaweza kusaidia kuimarisha usalama wa chakula na afya ya umma.

Takwimu zinaonyesha kuwa iwapo hatua sahihi kuhusu lishe bora hazitachukuliwa sasa, idadi ya watu wenye  uzito kupindukia duniani itazidi ile ya wenye njaa.

Kwa hivi sasa zaidi ya watu milioni 670 duniani ni tipwatipwa kulinganishwa na milioni 821 waliokuwa na njaa duniani kote mwaka 2017.

TAGS: FAO, WTO, WHO, utipwatipwa, usalama wa chakula, lishe bora