Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kubebwa muda mrefu, kuendeshwa kwenye vigari na kutumia skrini muda mwingi kwadumaza watoto- WHO

Kuongoza njia katika kufanya mazoezi ni mbinu bora ya kuvutia pia watoto nao kufanya hivyo
WHO
Kuongoza njia katika kufanya mazoezi ni mbinu bora ya kuvutia pia watoto nao kufanya hivyo

Kubebwa muda mrefu, kuendeshwa kwenye vigari na kutumia skrini muda mwingi kwadumaza watoto- WHO

Afya

Mwongozo mpya wa shirika la afya  ulimwenguni, WHO unatoa maelekezo ya jinsi ambavyo watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 wanatakiwa kucheza na kufanya shughuli zinazohusisha maungo yao badala ya kubebwa wakati wote au kutumia muda mwingi kwenye skrini za televisheni au michezo yao.

WHO inasema mwongozo huo unazingatia ukweli kuwa watoto wenye shughuli nyingi zinazohusisha maungo yao wana fursa kubwa ya kukua wakiwa na afya na hivyo suala la mazoezi lisiwe kwa watoto wa umri wa kati au barubaru na watu wazima bali pia kwa watoto wadogo.

Fiona Bull ambaye ni afisa wa WHO amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa “watoto wadogo wanapozaliwa tu wanakuwa na harakati zinazohusisha maungo yao lakini mifumo yetu ya maisha ndio inawaharibu. Mifumo ya kuwepo muda mwingi kwenye magari, matumizi ya vifaa vya kielektroniki na hivyo muda mwingi mtoto anakuwa ameketi.”

Amesema hiyo inaamaanisha kuwa mtoto hana fursa ya kukua kwa maungo yake na pia kiakili na anakosa fursa ya kucheza na marafiki zake, wazazi na wengine wote ambao ni muhimu.

MAENEO HUSIKA NA MWONGOZO

WHO inasema mwongozo huo unagusa  maeneo matatu ambayo ni muda wa kutumia vifaa vya eliktroniki ambavyo vina skrini, muda wa michezo ya viungo na pia kulala.

Dkt. Juana Willumsen ambaye anahusika na masuala ya utipwatipwa WHO amesema mambo hayo matatu yana uhusiano mkubwa hususan kwa watoto.

“Usingizi mnono unatoa hakikisho kuwa watoto wamepumzika vyema ili waweze kucheza na kujiendeleza. Muda ambao WHO unapendekeza wa michezo ni takribani saa 3 kwa siku.” Amesema Willumusen.

Hata hivyo amesema lazima wazazi ndio wawe mfano kwa watoto wao kupenda michezo, kupunguza muda wa skrini na pia kulala muda wa kutosha. “Muda wa kusimuliana hadithi, kusoma vitabu na watoto na kubadilishana mawazo na mlezi wa watoto ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto,” amesema Dkt. Willumsen.

VIPI SASA HATUA ZISIPOCHUKULIWA?

WHO inaonya kuwa kutozingatiwa kwa shughuli hizo tatu hivi sasa kunasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 5 kila mwaka.

Hivi sasa asilimia 23 ya watu wazima na asilimia 80 ya vijana barubaru hawako imara kimwili na hivyo, “iwapo utaratibu mzuri wa kutumia skrini, kufanya mazoezi na kulala utaanza mapema, hivyo utaweza kusaidia kujenga tabia hiyo kuanzia utotoni, ubarubaru hadi utu uzima.