Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya Watoto 40 wameuawa katika mashambulizi ya Sri Lanka:UNICEF

Bendera ya Sri Lanka (katikati) ikipepea katika viwanja vya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Bendera ya Sri Lanka (katikati) ikipepea katika viwanja vya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya Watoto 40 wameuawa katika mashambulizi ya Sri Lanka:UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, leo limesema limeshtushwa sana na kusikitishwa na ukatili wa hali ya juu ulioelekezwa kwa familia wakiwemo Watoto waliokuwa wamekusanyika makanisani na hotelini wakati wa siku ya Pasaka nchini Sri Lanka.

Shirika hilo limetoa pole kwa waathirika, familia na jamii zilizoathirika na mashambulio hayo ya kikatili.

Kwa mujibu wa shirika hilo taarifa kuhusu athari kamili za mashambulizi hayo kwa watoto na vijana bado zinaendelea kuwafikia lakini tayari wanafahamu kwamba idadi kubwa ya watoto wakiwemo raia wa Sri Lanka na wa kigeni wameuawa na kujeruhiwa, na wengine wako mahututi hospitali. UNICEF inasema hadi kufikia leo (Aprili 23 ) jumla ya watoto 27 wamepoteza maisha na 10 wamejeruhiwa kutokana na shambulio lililosababisha mlipuko mkubwa katika kanisa la Mtakatifu Sebastian mjini Katuwapitiya, Negombo. Huko Batticaloa, Watoto 13 wameuawa huku mdogo kabisa akiwa na umri wa miezi 18 tu na watoto 15 wakiwa na umri wa kati ya miaka 7 na 16 hivi sasa wanapatiwa matibabu hospitali.

Pia Watoto ambao ni raia wa kigeni 5 wamethibitishwa kuuawa. Katika mji mkuu Colombo watoto 20 raia wa kigeni wamelazwa hospitali huku wane kati yao wakiwa katika chumba cha wagonjwa mahtuti.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema watoto wengi wamepoteza wazazi ama mmoja au wote huku wengi wao wakishuhudia ukatili huo wa kutisha na kuoghofya.

Hivi sasa UNICEF inashirikiana kwa karibu na serikali ya sri Lanka ili kukusanya taarifa zinazoaminika kuhusu hali ya watoto na barubaru walioathirika na mashambulizi hayo.

Mahitaji ya watoto

Hadi kufikia sasa UNICEF imebaini mahitaji yafuatayo na inachukua hatua zinazostahiki.

Mosi :Baadhi ya hospitali ambako watoto wengi wamelazwa zinahitaji vifaa tiba na madawa na UNICEF iko katika mchakato wa kusaka na kufikisha vifaa tiba vinavyohitajika.

Pili: Watoto ambao wametenganishwa na wazazi au walezi wao wanahitaji msaada wa kubaini ndugu zao na kuunganishwa na familia zao. Na watoto ambao wamepoteza wazazi wanahitaji mahala pa kudumu pa kulelewa. UNICEF inatoa msaada wa kiufundi na fedha kwa huduma za muda ili kusaidia kuwaunganisha watoto hao na wazazi wao au kuwaweka kwa ndugu wa familia na walezi.

Tatu: Msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha umebainika kuwa moja ya mahitaji makubwa. Wiki hii UNICEF itakuwa inatoa msaada wa huduma ya kwanza wa kisaikolojia kwa watoto na familia zao ambazo zimeathirika.

Nne: UNICEF inaendelea kutoa msaada kwa wizara ya wanawake na watoto na wizara ya afya hasa kwa kuratibu masuala ya ukusanyaji wa takwimu na kuhakikisha kwamba watoto na barubaru wanpewa kipaumbele katika suala hilo.

UNICEF imelaani vikali ukatili huo ikisema hakuna mtoto anayestahili kuporwa maisha yake au mzazi anapaswa kupoteza mwanaye katika mazingira hayo. Mashambulizi hayo ya siku ya pasaka yamekatili Maisha ya watu zaidi ya 300.

Hanna Singer mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sri Lanka akizunguma na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis (2016)
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Hanna Singer mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sri Lanka akizunguma na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis (2016)

Hali halisi hivi sasa

Wakati huohuo mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sri Lanka Hanaa Singer akizungumza na Umoja wa Mataoifa kwa njia ya simu amesema “bado hivi sasa hisia ni za mshtuko na pia hofu.Tunazungumzia watu 310 wameuawa katika siku moja na wengine Zaidi ya 540 kujeruhiwa. Hivyo ni mshtuko mkubwa kwa nchi ambayo miaka kumi tu iliyopita ndio imetoka katika miaka 30 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Huu ni wakati wa kuwaomboleza waliokufa , mazishi yanafanyika leo na Kesho. Kuna hofu kubwa kwani hasira na jazba vinaongezeka vya kutaka kulipiza kisasi. Na kuna baadhi ya makundi yanaweza kulengwa kutokana na hili. Jamii nadhani bado siko katika hali ya taharuki na mshtuko na polisi wamepelekwa katika majimbo yote. “

Na kuhusu upande wa viongozi wa dini Bi. Singer amesema “Viongozi wa dini hadi sasa wamekuwa ni mahali pa usalama na wamekuwa wakitoa wito wa amani na utulivu.Viongozi wa makundi yote ya iamani tofauti za kidini wameshikamana kutoa wito wa kuwepo kwa amani na utulivu na serikali pamoja na jamii kwa pamoja wanaandaa mazishi na naeelewa kwamba jamii zote za Kiislam zimekuwa zikisaidia makanisa katika kuandaa mazishi. Hivyo bado kuna hofu kubwa watu wakisubiri hali ya kujibu mashambulizi.